Kuelekea miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), taasisi hiyo imezindua rasmi kampeni mahsusi ijulikanayo Kitabu Kimoja ili kufikia uwiano wa kila mwanafunzi kuwa na kitabu chake.
Akizindua kampeni hiyo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema lengo la kampeni hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi Kidato cha Sita ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.
“Taasisi hii ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 13 ya Mwaka 1975 kwa hiyo Juni mwaka huu inatimiza Miaka 50 toka kuanzishwa kwake. Katika kuadhimisha miaka 50, TET itafanya shughuli mbalimbali zinazoendana na majukumu yake makuu.
“Aidha, kupitia maadhimisho hayo, TET na ili kufikia lengo la Kampeni ya Mwanafunzi Mmoja Kitabu Kimoja, TET inawaalika wadau wote wa elimu nchini ikiwemo serikali, sekta binafsi, mashirika ya dini, mashirika ya kimataifa na watu binafsi katika kuchangia na kushiriki katika Matembezi ya Hisani ya tano yatakayofanyika Machi 7, kuanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Maktaba Mpya kupitia Chuo cha Maji, Mlimani City, Mwenge na kuishia Ofisi za TET Makao Makuu,” amesema Dkt. Komba.
Amesema mgeni rasmi katika matembezi hayo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim M. Majaliwa.
” Matembezi yataanza saa 12.00 alfajiri hadi saa 2.00 asubuhi na yatafuatiwa na hafla ya uzinduzi wa Sherehe za Miaka 50 ya TET itakayoanza saa 3:00 asubuhi katika viwanja vya TET Makao Makuu.
“Ili kushiriki wadau mnaombwa kujisajili na kuchangia Sh. 50,000 ambapo utapatiwa fulana au 150,000 (lutapatiwa trakisuti.
“Fedha zitakazopatikana zitaelekezwa moja kwa moja katika uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.
Ameitaja namba ya kuchangia moja kwa moja ni 994040118259, pamoja na mambo mengine, amesema taratibu za kuchangia na kujisajili zimebainishwa katika mitandao ya kijamii ya TET ya X, Instagram na Facebook inayopatikana kwa anuani ya taasisiyaelimutanzania.