Tenki la kuhifadhi maji linalojengwa katika mradi wa maji Kitula kata ya Kitula wilayani Mbinga.
Na Mwandishi Wetu,Mbinga
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,umeanza kutekeleza mradi wa maji ya bomba wa Kitula kata ya Kitula Halmashauri ya wilaya Mbinga utakaowaondolea wananchi wa kata hiyo kero ya kuamka usiku wa manane na kutembea umbali mrefu kila siku kwenda kutafuta maji na kuacha shughuli za kujipatia kipato.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala alisema,mradi wa maji Kitula unatekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 1.7 na utawanufaisha wananchi 9,100 wa vijiji vinne vya Mzuzu,Kitula,Mahilo na Lisau na utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 85.
Sinkala alitaja kazi zinazofanyika katika mradi huo ni ujenzi wa matenki matatu moja la lita 150,000 la pili la ujazo wa lita 100,000 la tatu lina uwezo wa kuhifadhi lita 75,000 na kulaza mabomba urefu kilometa 54.
Alisema, kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa matenki yote matatu na kujenga chanzo cha maji(Intake) na maji yameanza kufika kwenye matenki mawili kati ya matenki matatu kutoka kwenye chanzo.
Sinkala alieleza kuwa,wanasubiri mabomba ambayo yatalazwa urefu wa kilometa kumi ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo utanaotarajia kukamilika katika kipindi cha miezi minne ijayo.
Amewaomba wananchi, kuwa wavumilivu wakati huu ambapo Ruwasa kwa kushirikiana na mkandarasi inaendelea na jitihada za kukamilisha mradi huo haraka ili uanze kutoa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.
Diwani wa kata ya Kitula Alex Ngui alisema,mradi huo umewasaidia sana wananchi wa kata hiyo kupata huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yao na hivyo kupata muda mwingi wa kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo.
Ngui amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kuwa utaleta tija kubwa kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja,wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma hasa ikizingatia kuwa wananchi wa kata hiyo ni wakulima wakubwa wa zao la kahawa linalohitaji maji mengi.
Ameiomba Serikali, kuhakikisha inatoa fedha zilizobaki ili mkandarasi aweze kukamilisha kazi na wananchi waanze kupata huduma ya maji kwenye maeneo yao kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha badala ya kuendelea kutumia maji ya mito na visima vya asili.
Fundi anayesimamia mradi huo Said Mapembe,amehaidi kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati kwani kazi nyingi zilizopangwa kufanyika zimetekelezwa kwa asilimia kubwa.
Mkazi wa kijiji cha Mahilo Xveria Mhaiki,ameipongeza Serikali chini ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa uamuzi wa kujenga mradi huo katika kijiji cha Mahilo ambacho kwa muda mrefu wananchi wake wako kwenye mateso makubwa.