Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele
akitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili
majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo Tume itapokea mapendekezo kuanzia
Februari 27, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025. Tume ilitangaza uamuzi huo
muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chake maalum kilichokutanba
Mjini Morogoro leo Februari 26, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza kwa mchakato wa
kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo
itapokea mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26
Machi, 2025.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa
ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele leo tarehe 26 Februari,
2025 muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza kikao cha Tume kilichofanyika
mkoani Morogoro.
Kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 18(1) ya
Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, napenda kutoa
taarifa kwa umma kwamba, kuanzia kesho siku ya Alhamis tarehe 27
Februari, 2025 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itaanza mchakato wa
kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi, amesema
Jaji Mwambegele.
Akifafaunua kuhusu muda wa kupokea maombi, Jaji
Mwambegele amesema maombi yote ya kugawa au kubadilisha jina la jimbo
yawasilishwe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia tarehe 27 Februari,
2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.
Jaji Mwambegele amesema Tume
inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na kifungu cha 10(1)(d)
cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, ambapo
Tume imepewa jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano
katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.
Ameeleza
kuwa kwa mujibu wa ibara ya 75(4) ya Katiba, jukumu hilo la kuchunguza
mipaka na kugawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi linaweza
kufanywa na Tume mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka kumi.
“Kwa
kuzingatia masharti hayo ya Katiba, kwa mara ya mwisho Tume ilichunguza
mipaka na kugawa majimbo ya uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano mwaka
2015, ambapo majimbo mapya 26 yalianzishwa, amesema.
Jaji
Mwambegele amewakumbusha wadau wote wenye maombi wahakikishe kuwa
mapendekezo yanajadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Wilaya, kisha
yawasilishwe kwa Katibu Tawala wa Mkoa kwa ajili ya kujadiliwa katika
Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa awasilishe Tume
mapendekezo yaliyopitishwa na kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa pamoja
na viambatisho vyote.
Amesema vigezo vitakavyotumika ni wastani
wa idadi ya watu, ambapo kwa majimbo ya mjini ni kuanzia wastani wa watu
600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia wastani wa watu 400,000.
Ameongeza
kuwa, idadi ya watu itakayotumika ni ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa
ya Takwimu kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2022.
Jaji Mwambegele amevitaja vigezo vingine kuwa ni hali ya
kiuchumi ya Jimbo, ukubwa wa eneo la Jimbo husika, mipaka ya kiutawala,
jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa
maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa bunge, idadi ya
Wabunge wa Viti Maalum Wanawake, upatikanaji wa njia za mawasiliano na
hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.
Amesema
halmashauri zinazokusudia kubadili jina la jimbo zinatapaswa kufuata
utaratibu kama ule unaotumika katika kuwasilisha maombi ya kugawa
majimbo.
Sehemu ya wajumbe wa Management ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wakiwa katika mkutano huo maalum wa Tume. Sehemu ya wajumbe wa Management ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wakiwa katika mkutano huo maalum wa Tume.
Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele
(kushoto) akiongozana na wajumbe wa Tume wakitoka katika ukumbi wa
Mikutano Magadu Mkoani Morogoro leo Februari 26, 2025b baada ya kumaliza
kuongoza kikao cha Tume kilichofanyika mkoani Morogoro.