NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
WALIOKUWA Wafanyabiashara na wamiliki wa vibanda katika soko la Mbuyuni manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro lililoteketea kwa moto mwaka jana wameiomba serikali kuhakikisha inaisimamia manispaa ili kuwarejea vibanda vyao.
Hatua hiyo imekuja baada ya manispaa ya Moshi kulikarabati upya soko hilo kupitia mapato yake ya ndani.
Wafanyabiashara hao ambao waliunguliwa bidhaa zao wanadai kuwa mpaka sasa hawajui hatima yao katika soko hilo na kuiomba serikali kuhakikisha wanarejeshewa vibanda ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Moto wa mwaka jana ni mara ya tatu kuwaka katika soko letu hili na kutupatia hasara kubwa sisi Wafanyabiashara hivyo tunamuomba Mkurugenzi wa manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe atuangalie sisi tuliokuwa tukimiliki vibanda hivi hapo awali” Alisema mmoja wa Wafanyabiashara hao Peter Mselle.
Mselle alitumia nafasi hiyo kuipongeza serikali pamoja na manispaa ya Moshi kwa kutenga fedha kurejesha hali ya soko hilo ambalo linategemewa na Wafanyabiashara wengi katika mji wa Moshi.