Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imeshiriki Kongamano la 11 la Nishati ya Petroleum (EAPCE’ 25) kwa ajili ya kutoa elimu pamoja kutafuta fursa za ujenzi wa miundombinu ya umeme kwa wadau walioshiriki kutoka Nchi za Afrika Mashariki.
Kongamano hilo limefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ambapo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Machi 5 -7, 2025.
Akizungumza leo Machi 5, 2025 Jijini Dar es Salaam katika kongamano hilo lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Mhandisi Mkuu wa ETDCO Mustapha Himba, amesema kuwa lengo ni kuangalia fursa kwa makampuni kutoka Nchi za Afrika Mashariki ambazo zinatekeleza miradi ambayo inayohitaji miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa Umeme.
Mhandisi Himba amesema kuwa tumeamua kutumia fursa hii kwani itatusadia kupanua wigo njee ya nchi yetu kwani Kongamano hili limeunganisha nchi mbalimbali kutoka Africa.
Amefafanua kuwa ETDCO inaendela kutekeleza miradi mbalimbali nchini kwa ufanisi ikiwemo mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Mkoa wa Tabora hadi Katavi pamoja na miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Mkoa wa
Katavi, Mbeya Kigoma, Arusha, na Geita.