NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Atanas Paul, akimkabidhi Hamid Khatib Hamid boksi la tende wakati wa Ugawaji wa futari Kwa watoto Yatima wenye mahitaji maalum wanaolelewa Katika kituo cha ‘Zanzibar Aids association and support of orphans Mambosasa, kwaniaba ya Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindunzi, mama Mariam Mwinyi. ( PICHA NA FAUZIA MUSSA).
Na Ali Issa Maelezo
Mwenyekiti wa Maisha Bora Foundation Mama Mariam Mwinyi ametembelea na kutoa Msaada wa futari mbali mbali katika nyumba za Wazee wa Seblen na kituo cha kulelea watoto yatima Fuoni Mambo sasa.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Anna Athanas Poul katika vituo hivyo amesema ni kawaida ikifika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwatembelea wazee na watu wenye uhitaji maalum kuwasalimia na kuwapatia futari kwa ajili kujikimu.
Amesema wazee wanahitaji kutunzwa na kulelewa na kupatiwa mazingira mazuri kwa kuzingatia hali zao na mahitaji muhimu pamoja na kupewa chakula kizuri ili kuongeza faraja katika funga zao.
Ameeleza kuwa taasisi ya Mama Mariamu itandelea kuisadia jamii na kuwajali watu wenye mahitaji hasa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ili wapate fadhila na matumaini mazuri katika kutekeleza ibada ya funga.
Nae Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima Fuoni Mambo sasa Aboud Maulid Haji akipokea Msaada huo alimshukuru Mama Mariam Mwinyi kwa jitihada zake anazochukua kwa kuwatambua watoto wenye mahitaji malumu akiwa kama ni mlezi wao kwa kuwapatia msaada wa chakula cha Futari katika kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Watoto wangu ni wenye mahitaji maalum lakini wote wanafunga kwa kushindana kuazia miaka sita na kuendelea hivyo sadaka tuliyoipata itatusaidia sana katika kipindi hiki cha Ramadhani”, alisema Mkurugenzi huyo
Aidha alipongeza jitihada zinazofanywa Dkt. Mwinyi na Mama Mariamu kuimarika na kusaidia wananchi mbalimbali jambo ambalo linapaswa kushukuriwa na kuigwa na watu wengine kutoa sadaka zao katika kipindi hiki cha Ramadhani.
Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kuvitembelea vituo vya kulelea watoto yatima kwani kufanya hivyo kunatengeneza furaha mapenzi kwa watoto.
Amesema kituo chake kina watoto 48 wanaume 26 na 22 wakike ni watoto wenye uhitaji maalum ambao msaada huo utawasaidia kwa ajili ya kujikimu na kujiendeleza kimaisha
Msaada uliotolewa ni pamoja na unga wa ngano, sukari, tende, mafuta ya kupikia na mchele ambavyo vitasaidia futari katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.