WAKAZI wanne wa Jijjni Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu uchumi yenye mashitaka sita ikiwemo kukwepa kodi ya ushuru wa forodha na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh Milioni 125. 5
Mashtaka mengine ni kukwepa kodi kwa njia ya udanganyifu, kuchepusha mizigo kutoka kwenye njia iliyoidhinishwa, kutoa nyaraka ya uongo, kuondoa lakiri ya forodha, kuisababishia Mamlaka hasara na kupatikana na mali au bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru wa forodha.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali John Mwakifuna Akisaidiana na wakili Auni Chilamula na Emmanuel Medalakini amewataja washtakiwa kuwa ni Athanas Msenye, Maria Said, Godfrey Chamali na Polycap Haule.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Veneranda Kaseko imedaiwa kuwa, Februari 7, 2025 huko Mikocheni ndani ya Wilaya ya Kinondoni washtakiwa wote kwa pamoja walitoa tamko la uongo kwamba mzigo unaohusu vifaa mbalimbali vya magari ilikuwa safarini kuelekea DR Congo lakini wakaichepusha na kuilkezea eneo la Mikocheni Dar es Salaam hali ambayo ilisababisha ukwepa kodi wa zaidi ya Sh. Milioni 125,245,219.82
Katika shtaka la pili inadaiwa, siku na mahali hapo washtakiwa wote, walichepusha mzigo wa vifaa mbali mbali vya magari kutoka katika njia iliyokuwa imeidhinishwa kupita ya kutoka Dar es Salaam hadi Kongo na wao wakaupeleka mzigo huo eneo la Mikocheni.
Washtakiwa Msenye na Amina pia wanadaiwa Februari 7, 2025 huko katika bandari ya Dar es Salaam walitoa tamko la uongo kuhusu maelezo ya mzigo wa vipuri vya gari na kushindwa kujimuisha vifaa vya sola na taa.
Imeendelea kudaiwa kuwa, Februari 7,2025 huko Tabata Mwananchi, washtakiwa waliondoa lakiri ya forodha kutoka kwenye kontena la gari lenye namba za usajili ESDU 4263732.
Katika shtaka la tano inadaiwa washtakiwa wote Kwa makusudi, yaani kwa ulaghai wa walifanya kitendo cha kukwepa kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania hasara ya Sh. 125,245,219.81
Katika shtaka la sita inadaiwa kuwa Februari 7,2025 huko Mikocheni, washtakiwa Chamali na Haule walikutwa na vifaa mbali mbali vya gari huku wakijua kuwa vifaa hivyo havijalipiwa ushuru wa forodha na hivyo kukwepa kodi ya Sh. 125,245,219.82.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi itakapopewa kibali kutoka kwa DPP.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haijakamilika na umedai kuwa dhamana ya washtakiwa iko wazi, wameiomba Mahakama kutoa dhamana kwa mujibu wa sheria na masharti mengine ambayo Mahakama itaona yanafaa.
Hata hivyo, Hakimu Kaseko amesema amezingatia washtakiwa wanatuhumiwa na kesi ya Uhujumu Uchumi na kwa kuwa Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hatatoa masharti ya dhamana hadi pale kibali cha kuisikiliza kitakapotolewa
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 24, 2025 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa, washtakiwa wamerudishwa Mahabusu