Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika jijini Harare, Zimbabwe kuanzia tarehe 12 hadi 14 Julai, 2025.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao mbalimali ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali ikiwemo kutathmini utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza na yale ya Wakuu wa Nchi na Serikali pia utajadili Mpango wa Bajeti ya Jumuiya ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 hususan katika kutekeleza maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030.
Agenda za Tanzania za kipaumbele katika Mkutano huo ni pamoja na kuhimiza kufanyika kwa tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika Lugha ya Kiswahili baada ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Mhe. Prof. Dkt. Amon Murwira amesema umefika wakati sasa kwa Nchi Wanachama wa SADC kuwekeza katika rasilimali ilizojaliwa ikiwemo watu na maliasili ili kuiwezesha Jumuiya kufikia malengo iliyojiwekea kupitia program mbalimbali za maendeleo zikiwemo zile za viwanda na miundombinu ya kuinganisha kanda na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.
Amesema Baraza hilo limepewa jukumu la kusimamia ufanisi katika kanda kwa kuhakikisha kwamba sera zinaendana na dira ya SADC ya kuweka mbele maslahi ya watu wake kwa kuhakikisha maisha na vipato vyao vinabadilika, hivyo Mkutano huo uwe jukwaa ambalo litajadili na kuja na mapendekezo ya namna ya kujipanga kama kanda na kumiliki agenda yake ya maendeleo ikiwemo kuja na mikakati ya kutumia rasilimali lukuki zilizopo ikiwemo watu ili kupiga hatua za maendeleo zilizokusudiwa.
“Upatikanaji wa rasilimali fedha na nyingine zinazohitajika ni muhimu katika mustakabali wa Kanda yetu. Tunatakiwa kuunganisha nguvu zetu ili kutekeleza agenda zetu za maendeleo ikiwemo kukuza viwanda. Hii ni pamoja na kuongeza thamani kwa rasilimali nyingi tulizojaliwa na hapa nasisitiza kuwa, SADC tunayoitaka itajengwa na watu wake wenyewe” alisisitiza Mhe. Prof. Murwira.
Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi amesema bado suala la amani na usalama katika kanda linapewa kipaumbele ambapo jitihada za Nchi Wanachama zinaendelea katika kutafuta suluhu ya kudumu hususan katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumzia umuhimu wa nishati katika maendeleo ya Kanda, Bw. Magosi amesema jitihada zaidi zinahitajika ili kuwezesha takriban raia milioni 172 sawa na asilimia 29 wa SADC ambao wanaishi bila nishati ya umeme kufikiwa na huduma hiyo na kuutaja Mkutano kuhusu Nishati uliofanyika Tanzania mwezi Februari, 2025 chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kama moja ya hatua za mfano zinazopaswa kuchukuliwa katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Mbali na Waziri Shaaban, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Suleiman Hassan Serera, Mratibu wa Kitaifa wa masuala ya SADC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Baraza la Mawaziri ni chombo muhimu katika SADC ambacho kinahusika na kusimamia uendeshaji wa SADC ili kuhakikisha sera na maamuzi mbalimbali yanayofikiwa kwenye vikao yanafanyiwa kazi ipasavyo. Baraza hili linaundwa na Mawaziri kutoka Nchi Wanachama 16 za SADC, hususan kutoka katika Wizara zinazoshughulikia masuala ya Mambo ya Nje, Mipango na Fedha au Biashara, na hukutana mara mbili kwa mwaka.