NA DENIS MLOWE, IRINGA
KAMATI ya Ulinzi na Usalama Barabarani mkoa wa Iringa imekabidhi gari la kisasa kwa jeshi la polisi mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuimarisha doria za usalama barabarani.
Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Salim Abri (Asas) alisema kuwa gari hilo limetolewa na kamati hiyo baada ya kuongezeka kwa changamoto mbalimbali za barabarani hivyo gari hilo la kisasa litasaidia katika kuimarisha doria kwa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kazi nyingine za jeshi hilo.
Alisema kuwa gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser Deluxe limenunuliwa kwa sh milioni 100 kutokana na ada za ukaguzi na mchango kutoka kwa mwenyekiti wa usalama barabarani Salim Abri aliyechangia kwa kiasi kikubwa.
Aidha alisema wao kama taasisi muhimu ya Serikali wanawakaribisha wote wenye malengo ya kutoka misaada mbalimbali itayolisaidia Jeshi hilo kuzidi kuongeza ufanisi huku akisisitiza kuwa milango ipo wazi kwa wote wenye nia hiyo kama walivyofanya kampuni ya Vidam ambao wamtoa msaada wa pikipiki kwa jeshi hilo.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Usalam Barabarani, Glory Mtui alisema kuwa gari hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kwa kikosi cha usalama barabarani katika kufanya dolia za masafa mafupi na marefu na kutumika kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii inayotumia vyombo vya moto mkoani hapa.
Alisema kuwa ubora wa gari hilo licha ya kufanya doria litawezesha shughuli za ulinzi na usalama katika mkoa wa Iringa kufanyika kwa ufanisi zaidi.