Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Tanzanite ya Chusa Mining LTD, iliyoahidi kujenga wodi mbili mpya za wanawake na watoto na ofisi ya madaktari katika kituo cha afya Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, imefika eneo la tukio na kuonyeshwa mahali pa ujenzi.
Mdau wa maendeleo wa wilaya ya Simanjiro, Sporah Mwakipesile akizungumza na waandishi wa habari amesema Chusa mining LTD wameshaonyeshwa eneo la ujenzi huo na ramani yake.
Sporah amesema watajenga wodi ya wanawake, ya watoto na ofisi ya madaktari kwenye kituo hicho ambacho kina upungufu wa mahitaji hayo.
“Kampuni ya Chusa Mining LTD, imejitolea kujenga majengo hayo kwa lengo la jamii kupata huduma bora zaidi na kuondoa msongamano kwenye wodi za wanawake na watoto,” amesema Sporah.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani, Dkt Namnyaki Lukumay amesema wameshakabidhi ramani ya namna majengo hayo yatakavyojengwa.
Dkt Lukumay pia amesema wamekabidhi orodha ya mahitaji ya vifaa vya ujenzi (BOQ) kutoka halmashauri hiyo ili kampuni hiyo ianze ujenzi wake.
Amesema wodi hizo mpya zitasaidia jamii ya eneo hilo na majirani zao kupata huduma bora zaidi tofauti na hali ilivyokuwa awali.
Mwenyekiti wa kituo cha afya Mirerani, Twaha Mpanda ameishukuru kampuni ya Chusa Mining LTD kwa kujitolea kujenga wodi mpya ya wanawake, watoto na ofisi ya daktari kwani itapunguza msongamano.
“Wodi ya wanawake na watoto huwa inakuwa na watu wengi ila kupitia msaada huu wa kampuni ya Chusa itasaidia kuondoa msongamano huo,” amesema Mpanda.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, Rachel Njau ameipongeza kampuni ya Chusa mining kwa namna ilivyotekeleza ahadi hiyo kwa muda mfupi tangu watamke Machi 7 mwaka 2025.
“Tunaiomba serikali iwape ushirikiano sasa wasiweke vikwazo visivyo na msingi, kampuni imeamua kujenga ipewe nafasi isikwamishwe kwa lolote lile,” amesema Njau.