Na WMJJWM- New York Marekani
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewasilisha tamko la Tanzania kuhusu maendeleo ya nchi katika kufikia usawa wa kijinsia kwa kurejea Maazimio ya Beijing.
Waziri Dkt. Gwajima amewasilisha tamko hilo akiwa ni miongoni mwa Mawaziri wa nchi mbalimbali duniani waliowasilisha matamko rasmi ya nchi zao kwenye kipindi cha ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Hali ya Wanawake Duniani (CSW69), tarehe 13 Machi, 2025, Jijini New York Marekani.
Katika tamko hilo Waziri Dkt. Gwajima amesema katika utekelezaji wa maazimo ya Mkutano wa Beijing Tanzania imeongeza kwa idadi ya Viongozi Wanawake akimtaja Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mfano dhahiri katika hilo.
Amewataja Viongozi wengine wanawake kuwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika wa Bunge la Wawakilishi Zanzibar na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzbar. Aidha, pia alisema, kuna ongezeko la Wanawake Mawaziri, Wabunge, Makamisha, Majaji, Mabalozi na Madiwani.
“Wanawake Wajasiriamali wameendelea kustawi na wengi wameendelea kupata fursa za mitaji ambapo, mikopo nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 743.7 imeshatolewa kwa wajasiriamali hao huku kati yao wanawake wakiwa ni asilimia 52. Kwa upande wa Zanzibar, mikopo nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 31.6 imeshatolewa ambapo, asilimia 60 ilienda kwa wanawake” amesema Dkt Gwajima.
Dkt Gwajima ameeleza kwamba Sera ya elimu na mafunzo toleo la mwaka 2023 na mikakati yake imewezesha uwiano wa kuandikisha watoto shule za msingi kufikia 1:1 kati ya wasichana na wavulana, pamoja na Utekelezaji wa mikakati ya msingi na kina kwenye eneo la Wanawake na Afya ambapo vifo vitokanavyo na sababu za uzazi kwa wanawake vimepungua kutoka vifo 556 hadi 104 kwa vizazi hai 100,000.
Ameongeza kwamba Programu ya Afrika ya Wanawake na Nishati Safi ya Kupikia iliyozinduliwa kwenye Mkutano wa COP 28 chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kinara, na utekelezaji wa Mkakati kuhusu Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2023 -2033 unalenga asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Dkt. Gwajima amesisizitiza kwamba Tanzania imeboresha Sheria mbalimbali zikiwemo Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Mtoto ili kuwalinda Wanawake, Wasichana na Watoto. Pamoja na kuwa na sheria ya uchaguzi ili kupambana na ukatili dhidi ya Wanawake wakati wa uchaguzi na Vyama vyote vya Siasa.
Aidha, amesema tangu mwaka 2023 Tanzania inatekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo, imeshafikia watu milioni 1.3 huku nusu wakiwa ni Wanawake.