Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka Waandikishaji Wasaidizi na
Waendesha Vifaa vya Bayometriki (BVR) kutekeleza majukumu yao vituoni
kwa kufuata sheria, Kanuni na Taratibu za Tume pamoja na umakini katika
utunzaji vifaa.
Hayo yamesemwa leo Machi 14, 2025 na Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele
wakati alipotembelea na kuzungumza na washiriki wa mafunzo ya siku
mbili ya Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kwa
Jimbo la Ukonga Halmashauri ya Jiji la Daes Salaam.
“Katika
kufanya kazi ambayo kwayo mnafundishwa hivi leo, mkafanye kwa kufuata
Sheria, Kanuni na taratibu, vyote hivyo mtafundishwa lakini pale ambapo
utaona umekwama usisite kuwasiliana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
ili usikwamishe zoezi,” alisema Jaji wa Rufani Mwambegele.
Aidha,
Jaji Mwambegele aliwataka washiriki ambao ndio wanakwenda kutekeleza
jukumu la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Dar es
Salaam kuhakikisha wanatunza vifaa watakavyo kabidhiwa.
Jaji
Mwambegele alisema vifaa hivyo vimetumika nchi nzima kwa mizunguko 12
ambayo Tume iliipanga na sasa ipo mzunguko wa 13 unaotaraji kutekelezwa
Mkoani Dar es Salaam kuanzia Machi 17 hadi 23, 2025 kwa kutumia vifaa
hivyohivyo na vinapaswa kutunzwa kwani vitatumika pia katika awamu ya
pili ya zoezi la uboreshaji nchi nzima.
“Vifaa hivi isingekuwa
kutunza vyema msingekuwa hapa leo, vifaa hivi vimenunuliwa na kodi za
wananchi kwa bei ya juu sana hivyo nawaomba mvitunze vifaa hivi kwanza
wakati huu wa mafunzo lakini pili wakati wa zoezi lenyewe,” alisema Jaji
Mwambegele.
Akitembelea mafunzo kama hayo katika Halmashauri ya
Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es Salaam, Mjumbe wa Tume Mhe. Jaji Asina
Omari amewataka Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya
Bayometriki, kuzingatia mafunzo ya nadharia pamoja na vitendo ili
wakaweze kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Mapema akifungua mafunzo
hayo baada ya kuwaapisha washiriki hao kiapo cha kujitoa unachama na
kile cha kutunza siri, Afisa Mwandikishaji wa Jiji la Dar es Salaam,
Adv. Faraja Nakua aliwataka washiriki hao kufanya kazi kwa weledi na
kuwa na lugha nzuri kwa wananchi.
“Mtakapokua vituoni zingatieni
weledi wa kazi, nidhamu, kujituma na bidi ya kazi na lugha nzuri kwa
wateja wetu, wateja wetu ni Wapiga Kura watakao jitokeza kwaajili ya
kuboresha au kujiandikisha au kutoa taarifa za kufutwa kwa mpiga Kura
aliyepoteza sifa ya kuwepo kwenye Daftari,”alisema Nakua.
Mafunzo
hayo ya siku mbili yaliyoanza leo Machi 14 na kutaraji kutamatika Machi
15 mwaka huu ni maandalizi kuelekea zoezi la Uboreshaji wa daftari la
kudumu la wapiga kura Mkoa wa Dar es salaam kuanzia Machi 17 hadi
23,2025.
Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs
Mwambegele (katikati) akizungumza na washiriki wa mafunzo ya siku mbili
ya Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kwa Jimbo
la Ukonga Halmashauri ya Jiji la Daes Salaam alipotembelea mafunzo hayo
Machi 14,2025. Kulia ni Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, Ndg.
Gerald Sondo na Kushoto ni Afisa Mwandikishaji wa Jiji la Dar es
Salaam, Adv. Faraja Nakua. (Picha na INEC).
Waandikishaji
Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki kutoka Jimbo la Ukonga
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa wakila kiapo cha kujitoa uanachama
na kile cha kutunza siri leo Machi 14,2025 kabla ya kuanza kwa mafunzo
ya siku mbili kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
(Picha na INEC).
Baadhi
ya washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya Waandikishaji Wasaidizi na
Waendesha Vifaa vya Bayometriki kwa Jimbo la Ukonga Halmashauri ya Jiji
la Daes Salaam wakiwa katika mafunzo hayo. (Picha na INEC).