Na John Walter -Babati
Kijiji cha Sangaiwe, kilichopo katika Kata ya Mwada, kimenufaika pakubwa na juhudi za uhifadhi na kupiga hatua kubwa za maendeleo.
Kupitia uhifadhi, kijiji kimeweza kujenga miundombinu bora na kuboresha maisha ya wakazi wake kwa kiwango kikubwa.
Kijiji kimefanikiwa kujenga ofisi ya kisasa kwa ajili ya shughuli za utawala, jambo linalorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi huku kila kitongoji kikiwa na shule ya msingi.
Shule za kijiji zimepata madarasa mazuri na walimu wanaojitolea wanalipwa vizuri kwa juhudi za kijiji.
Matokeo mazuri yamerekodiwa, ambapo shule za msingi za kijiji zilishika nafasi ya kwanza na ya nne katika mtihani wa darasa la saba na la nne kwa ngazi ya mkoa mwaka 2024.
Kijiji cha Sangaiwe hupokea wageni 70-80 kwa siku, huku majirani zao wa Tarangire wakipokea zaidi ya 1,000 kila siku.
Kwa kutumia fedha za kijiji, zahanati imejengwa kwa zaidi ya shilingi milioni 200 na sasa ina vifaa tiba na dawa hatua ambayo imepongezwa mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda aliesema ujenzi wa zahanati hiyo ni muhimu kwa afya za wananchi.
Kwa muda mrefu, wakazi wa Sangaiwe wamekuwa wakikumbwa na changamoto za tembo wanaoharibu mazao yao jambo ambalo liliwasukuma kutoa mashamba yao kwa wawekezaji waliowekeza katika sekta ya malazi ya wageni.
Mwenyekiti wa bodi ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU), Patricia Mosea, amesema kijiji kimeanzisha hifadhi za jamii zinazohusisha vijiji 10 ili kubadilisha changamoto ya tembo kuwa fursa.
Wakazi sasa wanawaruhusu wawekezaji kujenga hoteli kwa ajili ya wageni wanaotembelea kijiji na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Wananchi wa Sangaiwe wameonyesha moyo wa uvumilivu kwani, licha ya tembo kupita kwenye makazi yao kila siku, wamejifunza kuishi nao bila bughudha.
Kwa kipindi cha miaka miwili, Shilingi Bilioni 2.4 zimeelekezwa kwenye shughuli za huduma za jamii kupitia mapato yatokanayo na utalii.
Hata hivyo, kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu sheria mpya ya mgao wa mapato kwani awali, vijiji vilikuwa vinapata asilimia 60 ya mapato kutoka kwa wawekezaji, lakini sheria mpya inataka wapewe asilimia 20 tu.
Diwani wa Kata ya Mwada Michael Mombo, pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Sangaiwe Mariani Mwanso, wamesema mabadiliko haya yanawavunja moyo wananchi na wanaomba serikali iendelee na mgao wa asilimia 60 ili kuhakikisha maendeleo ya kijiji yanaendelea kwa kasi.
Ujenzi wa shule, zahanati, na ofisi ya kijiji ni ushahidi wa jinsi uhifadhi unavyoweza kuinua maisha ya jamii.
Pamoja na changamoto ya tembo na mjadala kuhusu mgao wa mapato, wananchi wa Sangaiwe wanaendelea kufanikisha maendeleo yao kwa kauli mbiu ya Kata ya Mwada:
KAULI MBIU “Maendeleo Kwanza, Mambo Mengine Baadaye.” Tembo kwa Maendeleo.