Na. Mwandishi Wetu .
Wananchi
wa Mkoa wa Dar es Salaa wameanza Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura ambapo wananchi wengi walionekana kwa wingi vituoni
kujiandikisha au kuboresha taarifa zao.
Akizungumza jijini Dar
es Salaam leo Machi 17, 2025 baada ya kutembelea vituo vya Uboreshaji,
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Jacobs Mwambegele alisema zoezi hilo limeanza vyema pasi na
changamoto yeyote na kuwataka wananchi kuendelea kujitokeza.
“Tume
inaendelea na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na sasa
tupo mzunguko wa 13 mkoani Dar es Salaam, nimeshuhudia kuanza kwa zoezi
katika kituo cha Mnazi Mmoja…watu wengi wamejitokezakuja kujiandikisha
na kuboresha taarifa zao,”alisema Mhe. Jaji wa Rufani Mwambegele.
Jaji
wa Rufani Mwambegele amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa na
ameshauri wananchi wa Dar es Salaam kuzitumia siku za mwanzo za
uboreshaji ili kuepusha msongamano kwa siku za mwishoni mwa zoezi.
“Nawasihi
watanzania wale wanaostahili wajitokeze kwa wingi kuja kuboresha
taarifa zao au kujiandikisha, leo tarehe 17 mwezi huu wa tatu, 2025 ndio
siku ya kwanza mwisho tarehe 23 mwezi huu wa tatu 2025 sasa tunakawaida
ya kusubiri siku za mwisho hivyo nawasihi waje siku hizi za mwanzo,”
alisema Jaji Rufaa Mwambegele.
Nae Afisa Mwandikishaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye Majimbo ya Kawe na Kinondoni
Ndg. Omary Mkangama amesema zoezi hilo limeanza vizuri na hali ni shwari
na wananchi wanapata huduma vizuri.
Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi inataraji kuandikisha Wapiga Kura wapya 643,420 mkoani Dar es
Salaam ambapo jumla ya vituo 1,757 vinatumika kwenye uboreshaji kwa
mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96 katika vituo
1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Aidha
Tume imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wenye sifa za
kuandikishwa wanaandikishwa kwani BVR zaidi ya 5,000 na watendaji wa
kutosha wapo kwaajili ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Tume
imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 29. Kwa mujibu wa
ratiba, leo Tume inaanza uboreshaji katika mzunguko wa 13 ambao ni
mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu unahusisha
Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Kailima amesema kwa mkoa wa Dar es
Salaam Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni
sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 3,427,917 waliopo
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Tume inatarajia baada
ya uandikishaji Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura 4,071,337
idadi ambayo inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania
ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa
uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine
hawakuweza kujiandikisha.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari
linahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye
umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza
kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura
walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa
nyingine.
Uboreshaji wa Daftari pia unahusu kutoa fursa kwa
wapiga kura waliopo kwenye Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha
taarifa zao kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa
wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
Hawa Halifani Mbega mkazi wa Mtaa wa Mnazi
Mmoja Kata ya Jangwani Dar es Salaam akifurahia kadi yake mpya ya Mpiga Kura
baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji
Rufaa Jacobs Mwambegele. Mkoa wa Dar es
Salaam umeanza leo uboreshaji wa Daftari na utadumu kwa siku saba hadi Machi 23
mwaka huu. (Picha na INEC).
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,
Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele akimkabidhi kadi mpya ya Mpiga Kura Ndg. Hawa
Halifani Mbega mkazi wa Mtaa wa Mnazi Mmoja Kata ya Jangwani Dar es Salaam ambaye
alijitokeza wa kwanza kujiandikisha katika kituo cha Shule ya Msingi Mnazi. Mkoa
wa Dar es Salaam umeanza leo uboreshaji wa Daftari na utadumu kwa siku saba
hadi Machi 23 mwaka huu. (Picha na
INEC).
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,
Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele leo Machi 17, 2025 ametembelea baadhi ya vituo
vya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Dar es Salaam na
kushuhudia mwenendo wa zoezi hilo katiuka siku ya kwanza. Mkoa wa Dar es Salaam
umeanza leo uboreshaji wa Daftari na utadumu kwa siku saba hadi Machi 23 mwaka
huu. (Picha na INEC).