*KAGERA*
MADINI ya Bati (Tin) yameendelea kuwa na mchango kwenye maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini mkoani Kagera huku watanzania wakitakiwa kuchangamkia fursa za uchimbaji wa madini hayo.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kagera, Nobert Mkopi amesema, mkoani Kagera kuna fursa nyingi zikiwemo za huduma za maabara kuweza kufanyia uchunguzi wa madini yanayopatikana, makampuni ya ulinzi kwenye migodi na wafanyabiashara wakubwa wa Madini, makampuni ya uuzaji mitambo pamoja na fursa za leseni za uchimbaji mdogo na mkubwa.
“Watu waje wawekeze kwenye uchimbaji wa madini ya Bati, maeneo bado yapo mengi katika maeneo ya Nyaruzumbura , Katera , Murongo n.k wilayani Kyerwa, uchimbaji unaoendelea ni mdogo wa maduara, wachimbaji wakubwa kutoka ndani na nje tunawakaribisha,”amesema Mkopi na kuongeza,
“Soko la Madini ya Bati linakua, kwa sasa madini hayo yameendelea kuchangia katika maduhuli yatokanayo na Sekta ya Madini mkoani hapa,”amesema.
Amesema, madini ya bati yana matumizi mbalimbali ikiwemo kutumika kuunganisha vitu mbalimbali kama mabomba ya chuma na metali (Steel/ Metal), mifumo ya umeme (electric circuit), mifumo ya kielektroniki ya simu, vyuma vya reli, mifumo ya ndege na mifumo ya lifti za umeme kwenye ghorofa.
Pia, madini hayo hutumika kuzuia kutu kwenye vyombo vya kuhifadhia vyakula kwa muungano wa madini ya chuma. Bati vilevile hutumika kuzuia kutu kwenye mabati ya kujengea nyumba.
Aidha, Mkopi akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini hayo amewataka kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali na kupiga marufuku utoroshaji wa madini.
“Wachimbaji wa haya maeneo mmepewa leseni mchimbe kwa kufuata sheria na miongozo ya Serikali, na kinachopatikana kiingie kwenye mfumo sahihi, atakayepatikana anachepusha madini yetu kupeleka nchi nyingine bila utaratibu, atachukuliwa hatua za kisheria,” amewatahadharisha Mkopi.
Naye mchimbaji Evalista Didas akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wa madini ya Bati katika eneo hilo la Murongo lililopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera, amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwaamini na kuwapa leseni za uchimbaji.
“Serikali imetuwekea mazingira mazuri ya uwekezaji na soko, zamani madini haya yalikuwa hayafahamiki kilo tuliuza Shilingi 2,000 lakini sasa hivi tunauza Shilingi 40,000 tuna mafanikio makubwa katika uchimbaji wetu,”amesema Didas na kuongeza,
“Siku za nyuma wachimbaji tulikuwa tunadharaulika, mtu akikuona unatoka kuchimba anakudharau, lakini sasa hivi akikuona unatoka kuchimba anakuona wa thamani, tunasomesha, tumejenga, tunafuga kwa pesa tunazopata katika madini haya ya bati” amesema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyaruzumbura, Kata ya Nyaruzumbura kilichopo Mrongo , Zaid Silaji akizungumza amesema kijiji chao wamefaidika kutokana na wawekezaji wa Sekta ya Madini katika shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi na Sekondari za Nyaruzumbura, ujenzi wa ofisi ya serikali ya kijiji na wamefufua barabara ambazo zilikuwa hazipitiki.
‘Kwa sasa hatuna tena changamoto ya barabara, Sekta ya Madini kwenye kata yetu ni mkombozi, kikubwa tunachoomba Serikali kupitia Ofisi za Madini kutupa semina mbalimbali wananchi ili tutambue fursa zaidi zilizopo katika maeneo yetu na kuzithamini,”amesema Silaji.