Na mwandishi wetu
Benki ya NMB imeshiriki na kudhamini Jukwaa la Kujadili Masuala ya Maji lililofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayoendelea nchini. Jukwaa hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya maji ili kujadili mustakabali wa usimamizi, uhifadhi, na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, aliongoza mkutano huu wa wadau, ambapo benki ya NMB iliwakilishwa na Meneja Mahusiano Mwandamizi wa Huduma za Serikali, Irene Masaki. Katika mkutano huo, Bi. Irene alieleza jinsi NMB inavyojikita katika kusaidia miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta ya maji, kupitia huduma zake za kifedha zinazolenga taasisi za umma na sekta binafsi.
Mbali na kushiriki mijadala, NMB pia imepata nafasi ya kutoe elimu kuhusu huduma na suluhisho yake kwa washiriki wa mkutano huo, ikilenga wadau wa sekta ya maji kupata ufumbuzi wa kifedha kwa ufanisi zaidi.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka huu yanafanyika kwa mtazamo mpya, yakihusisha mikutano ya kitaalamu na mapitio ya sekta ili kutathmini maendeleo katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira. Katika kuunga mkono jitihada hizi, Benki ya NMB inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa.