Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 30 ya VETA jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kassore akitoa maalezo kuhusiana na mikakati ya VETA kwenye maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akitoa maelezo kuhusiana na maendeleo na mafanikio ya maadhimisho ya miaka 30 ya VETA jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali katika maadhimisho ya miaka 30 ya VETA.
*Kuendana na Mabadiliko ya Teknolojia
Na Chalila Kibuda,Michuzi Tv
SERIKALI imesema kuwa katika maadhimisho ya miaka 30 ya VETA inahitaji kutafakari katika kwenda mabadiliko ya Teknolojia katika utoaji mafunzo.
Hayo ameyasema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Maadhimisho ya miaka 30 ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema kuwa mafunzo ya ufundi Stadi yameajiri watanzania katika sekta binafsi na kutoa mchango wa maendeleo ya nchi.
“Mafunzo ya ufundi stadi yatolewe kueandana na mabadiliko ya teknolojia, mafunzo hayo yajumuishe ujuzi wa teknolojia za kisasa zinazochochea uzalishaji wenye tija”amesema
Aidha amesema katika utoaji wa mafunzo ya ufundi Stadi Serikali inatambua mchango wa wadau mbalimbali ya kufanya VETA kuwa tegemeo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna vyuo vya Ufundi Stadi 825 ambavyo vinamilikiwa na watu binafsi, na serikali ina vyuo 80 hivyo jumla ya vyuo vyote nchini ni 905.
“Tunawapongeza wadau mbalimbali kwa kuunga mkono jitihada za serikali kwenye sekta hii ya Ufundi Stadi, takwimu zinaonesha hadi sasa kuna vyuo vya Ufundi Stadi 825 ambavyo vinamilikiwa na watu binafsi, na serikali ina vyuo 80 hivyo jumla ya vyuo vyote nchini ni 905,” amesema Majaliwa.
Hata hivyo amesema kuwa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonesha kuwa takribani asilimia 70 ya ajira zote ni ajira binafsi na kwa watu wenye elimu ya ufundi stadi hasa kwenye sekta za kilimo, ujenzi, usafirishaji, na huduma za kijamii.
“Kwa upande wa nchi yetu, takwimu za ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2020 na 2024 zinafikia Milioni saba ambapo ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi imeajiri watu milioni 6.1 sawa na asilimia 87.1 ambapo wengi wao wana elimu ya ufundi stadi, na sekta rasmi imeajiri watu 907,873 (asilimia 12.9) ambapo wengi wao ni wale wenye elimu ya juu,” amesema Majaliwa.
Aidha Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini watoe mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Mahitaji ya soko la ajira tutayajua kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa.”
Amesema katika zama hizi zenye kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa VETA kuendelea kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara wahakikishe ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi unakamilika haraka.
Waziri Mkuu amesema ukamilishwaji wa vyuo hivyo vinavyojengwa na Serikali unalenga kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania kiujuzi.
“Ujenzi wa vyuo hivi ukikamilika, VETA itakuwa na vyuo 145 katika ngazi ya Mikoa yote 26 na Wilaya zote nchini. Vilevile, katika vyuo 80 vilivyopo, vyuo 30 vilikamilishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (6). Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa anayowafanyia Watanzania.”
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema wanaendelea kutekeleza agizo la Rais Samia wa ujenzi wa VETA katika wilaya zote nchini.
“Pamoja na hili pia tunazidi kuimarisha mfumo wa utoaji wa elimu kwa kuendana na mazingira. Pia kuimarisha mahusiano kati ya VETA, wazalishaji na Viwanda,” amesema Profesa Mkenda.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa VETA, CPA Anthony Kasore amesema wataendelea kutoa elimu hiyo ya Ufundi Stadi pamoja na kusimamia bunifu na Teknolojia mbalimbali.
“Tunaishukuru serikali kwa kuzidi kuweka mkazo ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa na ujuzi ambao utamwezesha kupata kipato. Pia wananchi waendelee kutuamini katika kuwapa ujuzi na maarifa,” amesema CPA Kasore.