Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa wilaya ya Butiama, mkoani Mara, yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CRDB, TCB, NMB na NBC.

Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa elimu ya fedha kupitia vipeperushi vyenye mada mbalimbali ikiwemo akiba, uwekezaji, mikopo walizofundishwa wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa baaadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wilayani Butiama, mkoani Mara, yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CRDB, TCB, NMB na NBC.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wakazi wa Kijiji Kyankoma, Kata ya Nyamimange, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yenye mada mbalimbali ikiwemo masuala ya mikopo, akiba na uwekezaji yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CRDB, TCB, NMB na NBC.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, Bw. Zakaria Wambura, akiuliza swali namna ya kuitambua Taasisi iliyosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi nyingine za Serikali mkoani Mara, ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CRDB, TCB, NMB na NBC.

Afisa Mikopo wa Benki ya CRDB, Bw. Calvin Temba, akieleza mikopo ya vikundi inayotolewa na benki hiyo kwa wananchi walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi nyingine za Serikali mkoani Mara, ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CRDB, TCB, NMB na NBC.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Butiama Mara).
…………..
Na. Josephine Majura, WF, Mara.
Wakopaji wametakiwa kutojihusisha na matumizi ya dhamana za mali za familia bila ridhaa ya familia husika ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea iwapo mali hizo zitapotezwa kutokana na kushindwa kulipa mikopo.
Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa kwa wananchi wa Kijiji cha Kyankoma, Wilaya ya Butiama mkoani Mara na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF pamoja na Taasisi za Benki, ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC.
“Wakopaji wanatakiwa kuwa waangalifu na kuhakikisha wanaelewa masharti ya mikataba ya mikopo kabla ya kutumia mali ya familia kama dhamana ili kuhakikisha kuwa dhamana zinazotolewa hazihatarishi ustawi wa familia” alisema Bw. Myonga.
Aliongeza kuwa Taasisi za kifedha zinatakiwa kuwa waangalifu na kufuata sheria na taratibu stahiki kabla ya kukubali mali ya familia kuwekwa kama dhamana, kwa kuhakikisha kuwa hati zote muhimu, kama vile hati za umiliki na ridhaa za maandishi za familia husika vinaambatishwa.
Akizungumzia kuhusu udhamini wa mkopo, Bw. Myonga, waliwashauri wananchi kabla ya kukubali kuwa wadhamini, wahakikishe wamejiridhisha kuwa mkopaji ana uwezo wa kulipa mkopo kwa wakati.
Alifafanua kuwa mtu akiwa mdhamini, anakuwa na wajibu wa kulipa mkopo wote endapo mkopaji atashindwa kulipa jambo ambalo linaweza kuathiri mali zake binafsi na hali yake ya kifedha.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Bi. Rebeca Sanga, aliwasisitiza wanavikundi wote nchini kusimamia vizuri miradi waliyonayo ili izalishe faida kwa ajili ya manufaa ya kundi na mtu mmoja mmoja.
Aliongeza kuwa miradi ya kikundi ikisimamiwa vizuri itazalisha faida ambayo inaweza kutumika kama mtaji wa kukopeshana wanakikundi na kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha Bw. Bryan Mkurya, aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi zote kuanzia Kitongoji hadi Kata ili kuhakikisha kila mwananachi anapata elimu ya fedha.
Aliongeza kuwa Serikali ihakikishe inatoa elimu kwa mkopaji na mkopeshaji ili wote wawe na uelewa wa pamoja ili kupunguza migogoro inayoendelea nchini.
Bw. Mkurya aliishauri Serikali kutumia mikusanyiko mbalimbali kutoa elimu ya fedha ikiwemo nyumba za ibada na mikusanyiko mingine inayotambulika na Serikali ili iweze kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja.