Dar es Salaam, 19 Machi 2025 — Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Mhe. Hamza S. Johari, amesema kuwa Ofisi yake imejizatiti katika kuhakikisha
inaendelea kuboresha uwezo na utendaji wa Mawakili wa Serikali nchini, ikiwa ni
sehemu ya juhudi za kukuza umahiri na weledi katika utoaji wa huduma za
kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum
uliofanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam,
Mhe. Johari alibainisha kuwa mafunzo ya kitaalamu kwa Mawakili wa Serikali
yatafanyika Arusha kuanzia tarehe 24 hadi 28 Machi 2025. Mafunzo haya yamelenga
kuwawezesha mawakili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila
siku.
“Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa kuendeleza wataalamu wa
kisheria ndani ya Serikali, sambamba na kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria,”
alisema Mhe. Johari.
Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele
kusisitiza umuhimu wa kuwa na Mawakili wa Serikali wenye ujuzi wa hali ya juu
ili waweze kulinda vyema maslahi ya taifa, hasa wakati huu ambapo Tanzania
inafungua milango kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu, mafunzo hayo yataendeshwa na
wakufunzi waliobobea kutoka ndani na nje ya nchi, huku mada zitakazotolewa
zikigusa maeneo muhimu kama vile uandishi na majadiliano ya mikataba ya
kimataifa, usuluhishi wa migogoro ya biashara, pamoja na uandishi wa sheria.
“Tunahitaji kuwa na wanasheria wanaoendana na kasi ya ukuaji
wa uchumi na uwekezaji. Ni lazima tuwe na maarifa ya kutosha katika maeneo kama
masoko ya fedha, masoko ya mitaji, sheria za fedha za kigeni na masuala ya
dhamana na hati fungani,” alieleza.
Katika kuimarisha uzalendo na kulinda maslahi ya taifa, Mhe.
Johari alisema kuwa mafunzo haya pia yatakuwa jukwaa muhimu kwa Mawakili wa
Serikali kujitathmini na kujijengea utayari wa kutoa huduma zenye tija kwa
nchi.
Akihitimisha, Mhe. Johari aliwahimiza Mawakili wote wa
Serikali ambao bado hawajajisajili kwa ajili ya mafunzo hayo kuhakikisha
wanakamilisha usajili wao mapema, huku akizitaka Wizara, Taasisi na Halmashauri
kuhakikisha zinawaruhusu mawakili wao kushiriki ipasavyo.
“Natoa wito kwa Mawakili wa Serikali kote nchini kuhakikisha
hawakosi kushiriki mafunzo haya muhimu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mhe. Johari alitumia fursa hiyo
kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, kwa kutimiza miaka minne ya mafanikio makubwa tangu alipoingia
madarakani, akieleza kuwa uongozi wake umeleta mabadiliko chanya katika sekta
mbalimbali nchini.