Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amewataka wadau wa madini kuwekeza miradi mbalimbali kwenye eneo hilo ili kuzidi kuinyanyua Manyara kiuchumi.
Mnyawi ameyasema hayo kwenye kikao cha kamati tendaji ya MAREMA, kilichofanyika katika ofisi za makao makuu yake yaliyopo mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro.
Amesema wadau wa madini kwenye Mkoa wa Manyara, wanapaswa kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuzidi kunyanyua uchumi wa Manyara na kutoa ajira.
“Hivi karibuni wadau wa maendeleo mbalimbali tulikutana na Mkuu wetu wa Mkoa wa Manyara, Mhe Queen Sendiga, tukazungumza juu ya agizo lake la wadau wa madini kuwekeza Manyara,” amesema Mnyawi.
Amesema siyo vyema wadau wa madini wa Manyara, kufanya shughuli zao na kupata faida wakiwa Manyara na kushindwa kuwekeza kwenye mkoa huo ili uzidi kupiga hatua kwa maendeleo.
“Mkuu wetu wa Mkoa amesema endapo mtu anataka kufanya uwekezaji mkubwa ikiwemo vituo vya mafuta, hoteli za kitalii, shule na maendeleo mengine ataweza kupatiwa ardhi bure ili awekeze,” amesema Mnyawi.
Amesema suala la wadau wa madini kuwekeza Manyara, linapaswa kuzungumzwa kwa wote, ili lieleweke kwa watu wa sekta hiyo kwani wanachumia Manyara hivyo wawekeze Manyara.
Makamu Mwenyekiti wa MAREMA, Money Yusuph ameunga mkono suala hilo kwa kusema kuwa wadau wa madini wakiwekeza miradi mingi ya maendeleo Manyara itazidi kupita hatua.
“Naunga mkono hoja hiyo ya wadau wa madini kuwekeza kwenye Mkoa wetu wa Manyara, kwani hapa ndipo tunapopata mazao yetu napo panapaswa kunufaika,” amesema Money.
Mweka hazina wa MAREMA, Neney John Lyimo amesema wadau mbalimbali wa maendeleo wanapaswa kuiga mfano wa Mwenyekiti mstaafu wa MAREMA Justin Nyari aliyejenga shule.
“Mwenyekiti mstaafu Nyari alifanya uwekezaji mzuri Manyara kwa kujenga shule nzuri ya mchepuo wa kiingereza ya Glisten Pre & Primary iliyopo mji mdogo wa Mirerani,” amesema Lyimo.
Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Nadonjukin, Swaleh Abdalla amesema ushauri huo wa wadau wa madini kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye mkoa huo ni wa kuungwa mkono.