Na Khadija Kalili Michuzi TV
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT ) Mary Chatanda ametoa rai kwa wanawake wote nchini kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea katika ngazi za Udiwani na Ubunge kwenye uchaguzi mkuu ujao hukulengo likiwa kumpa ushindi wa kishindo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo nawaomba wanawake mjitokeze kwa wingi katika kugombea nafasi za Udiwani na Ubunge lakini pia kujipanga kumuunga mkono mwanamke mwenzetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan twendeni tukavunje rekodi ya kumchagua Rais mwanamke kwa mara ya kwanza nchini na kumchagua kwa kura ningi ndani ya boxi” amesema Chatanda.
“Katika kufanikisha ushindi huu wa kishindo kila mmoja wenu ahakikishe yumo katika daftari la wapigakura 2025 shime kwa ambao bado hawajajiandikisha wajitokeze kwenye zoezi la uandikishaji kwenye Daftari la mpiga kura. itikadi za vyama nitasimama kidedea anashinda hivyo ingieni kwenye majimbo kwa kifua mbele mimi nitapanda juu ya meza kuhakikisha majina yenu yanarudi” amsesema Mwenyekiti wa UWT Chatanda.
Chatanda amesema hayo jana usiku tarehe 22 Machi 2025 alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya usiku wa Huba Huru Gala iliyokua na kaulimbniu isemayo ‘Acha Upendo Utawale’ iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Superdome Masaki Jijini Dar es Salaam.
Chatanda amesema kuwa anawapongeza uongozi wa Clouds Media Group na heshima za kipekee ziende kwa Mkurugenzi Mtendaji wake Joseph Kusaga kwa kumualika kuwa mgeni rasmi sambamba na kufanikisha hafla hiyo.
“Nawapongeza sana CMG kwa kuendelea kuwa wabunifu wa kuandaa hafla mbalimbali nchini na zenye mlengo wa kujenga zaidi kizazi cha wanawake hasa kiuchumi,kifikra na kijamii” amesema Mwenyekiti huyo.
“Leo ni siku ya kipekee tena ikiwa ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa ndugu zetu waislam na pamoja na wakristu ambao wako kwenye mfungo wa Kwaresma wote tumekutana hapa siyo tu kwa sherehe bali kwa dhamira thabiti ya kuweka ahadi mpya kwa mustakali wa wanawake wa Tanzania.
“Hafla hii imelenga kutukutanisha wanawake kutoka kada mbalimbali bila kujali itikadi za vyama,dini ,rangi zetu na makabila yetu imekuja wakati sahihi kwani sote tunatambua kuwa wanawake ni Jeshi kubwa na kwa hapa nchini tuko wengi zaidi kuliko wanaume kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 takriban asilimia 51 ya watanzania ni wanawake” amesema Chatanda.
Amesema kuwa “Tunasimama hapa kama wawakilishi wa kizazi cha sasa cha wanawake tukiwa na dhamana ya kuwaongoza dada, binti na mama zetu kuelekea kwenye umoja thabiti wa maendeleo na ustawi wa jamii yetu kwa ujumla.
“Usiku huu ni usiku wa mabadiliko tumekusanyika hapa siyo kwa burudani tu bali kwa sababu ya kutimiza jukumu kubwa tulilonalo kama wanawake wa taifa hili kwani kuna msemo usemao ukiwawezesha wanawake umestawisha taifa” amesema Chatanda.
“Tunahitaji kukomesha dhana potofu kuwa adui wa mwanamke ni mwanamke kauli hii haijawahi kuwa kweli na leo tunathibitisha kuwa sisi ni nguzo ya maendeleo siyo maadui wa maendeleo baina yetu na sasa rafiki wa mwanamke ni mwanamke mwenziye tukishirikiana , tukisaidiana na tukiamini katika uwezo wetu hakuna linalotushinda”
amesema Mwenyekiti huyo .”Historia imethibitishwa kuwa pale ambapo wanawake wameungana maendeleo yamekuwa dhahiri na mshikamano wetu ndiyo unajenga nguvu ya jamii “.
“Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametimiza miaka minne tangu ailipoingia madarakani tumeshuhudia akipongezwa kila kona ya nchi hii na shuhuda mbalimbali za kazi kubwa na nzuri iliyofanyika katika kipindi hiki , Rais wetu ametuheshimisha wanawake wa nchi hii, Bara la Afrika na ulimwengu kwa ujumla kwa kupitia aina ya uongozi wake unaozingatia 4R na sisi ni mashuhuda hapa mara tatu mfululizo ametajwa kuwa miongoni mwa wanawake100 duniani wenye ushawishi, amepata tunzo nyingi ndani na nje ya nchi hakika amekuwa kinara wa mageuzi makubwa katika kujenga kizazi chenye usawa wa kijinsia nchini kwetu”amesema Chatanda.
“Baadhi ya juhudi zake ni pamoja na kuanzisha mfuko wa maendeleo ya Wanawake (WDF) ambao umewezesha wanawake wengi kupata mitaji ya biashara, mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri isiyo na riba kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambayo imesaidia makundi haya hasa katika ngazi za vijiji, kata kupata uwezeshaji, kuwezesha makundi maalum wakiwemo wamachinga kutambulika kuwajengea miundombinu kuwatafutia fursa za kibenki na zenye riba nafuu” amesema Chatanda.
“Amewawezesha wasanii kupata mfuko wa kuwakopesha na kuwatafutia fursa mbalimbali nje ya nchi mfano ziara yake aliyofanya nchini Korea, kuimaarisha sekta ya afya ya uzazi kwa kuhakikisha huduma bora za mama na mtoto zinapatikana kwa urahisi zaidi kupitia ujenzi wa miundombinu ya sekta ya Afya na uwepo wa vifaa tiba vya kisasa hali iliyopelekea kupunguza vifo vya wanawake wajawazito mama kutoka 556 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000 na kwa upande wa watoto wachanga vifo vimepungua kutoka vifo 67 kati ya vizazi 1,000 hadi 43 kwa vizazi hai 1,000 na matokeo haya yamemwezesha Rais wetu kutunukiwa Tunzo ya Goal Keeper Award ” amesema Chatanda.
“Tunzo hii ni heshima kwa wanawake waliovunja mipaka na kufanikisha maendeleo makubwa katika jamii zetu tuendelee kusherehekea, kuthamini na kuenzi mchango wa wanawake wa Tanzania” amesema Chatanda.
Aidha Chatanda ametoa pongezi kwa Kampuni ya Clouds Media Group kuwa wameandika historia Barani Afrika kuwa na Redio ya Wanawake pekee inayofahamika kwa jina la Malkia Choice FM inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Juhaina Kusaga, kuwa imedhihirisha dhamira ya kweli ya Clouds Media Group katika kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwa sauti ya wanawake wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Hafla hiyo ya Usiku wa wa Huba Huru imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni Rehema Kyando kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambapo amewaasa wanawake kuwa na utamaduni wa kuwekeza kwa kujiwekea akiba na kukuza mitaji na kuacha kununua vitu vya anasa.
Wengine waliohudhuria ni viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga , Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Subira Mgalu wanawake wasanii kutoka vikundi mbalimbali huku wafanyabiashara Jiji la Dar es Salaam wamemchangia Rais DKT.Samia Suluhu Hassan kiasi cha Mil.700 kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.