Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) imekutana na viongozi wa Kampuni ya Uwakala ya Apex Ltd katika ukumbi wa ZMA, Malindi, kwa lengo la kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni hao, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa ZMA, Harieth Limo, alisema mamlaka hiyo iko tayari kupokea elimu kuhusu shughuli za uwakala zinazoratibiwa na Apex Ltd ili wafanyakazi wa ZMA wapate fursa ya kuzitumia huduma zinazotolewa na wakala huyo.
Aidha, Harieth alieleza kuwa jamii ya Zanzibar awali ilikuwa na mashaka kuhusu shughuli za Apex Ltd kutokana na taarifa mbalimbali zilizokuwa zikisambaa. Hivyo, ZMA iliona ni vyema kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu kazi zinazofanywa na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Apex Ltd tawi la Zanzibar, Mundhir Abdalla Said, alisema kampuni hiyo inasimamia huduma mbalimbali za uwakala, ikiwemo bima, umiliki wa viwanja, utayarishaji wa pasipoti na visa, pamoja na uratibu wa safari za kutembelea maeneo ya kitalii.
Mundhir aliongeza kuwa Apex Ltd imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar, hasa katika sekta ya umiliki wa ardhi, ambapo awali wananchi walikumbana na changamoto kama utapeli wa kuuziwa viwanja mara mbili na kasoro nyingine za umiliki wa ardhi.
Wakati wa mkutano huo, wafanyakazi wa ZMA waliomba ufafanuzi zaidi kuhusu aina za bima zinazotolewa na Apex Ltd, aina za viwanja wanavyosimamia, pamoja na namna kampuni hiyo inavyowasaidia wananchi wanaopata ajali barabarani.
Apex Ltd inaendelea kutoa huduma zake katika Jengo la Thabit Kombo, Michenzani, ikiwa na dhamira ya kusaidia wananchi wa Zanzibar kwa kuwapatia huduma za bima, usajili wa viwanja, hati za kusafiria, na safari za kitalii.