Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Khamis Mwinjuma, akikata utepe kuzindua uwanja mpya wa Airtel Stadium utakaotumiwa na Klabu ya Singida Black Stars mkoani Singida hivi karibuni. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Makete Festo Sanga, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Airtel Tanzania, Franky Filman (wa pili kulia); Mkurugenzi wa Biashara wa Bnki ya NBC, Elvis Ndunguru na Mwenyekiti wa timu ya Singida Black Stars, Ibrahim Mirambo (wa kwanza kulia).
Singida, Machi, 2025:
KAMPUNI ya Airtel Tanzania imefanya jambo la kipekee katika sekta ya michezo na burudani kwa kuzindua uwanja mpya wa mpira wa miguu uitwao Airtel Stadium, mkoani Singida.
Lengo kuu ni kusaidia kutatua changamoto ya miundombinu muhimu ya michezo nchini kama sehemu ya kuchochea ukuaji wa mchezo wa mpira wa miguu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uwanja huo mpya uliojengwa na Airtel kwa kushirikiana na Singida Black Stars, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Tamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma (mwanafa) aliipongeza Airtel kwa ujenzi wa uwanja huo huku akitoa wito kwa wananchi wa Singida kuutunza uwanja huo.
“Niwashukuru wadau wote waliofanikisha uwanja huu kuwa katika sura, niwashukuru Airtel, na wadau wengine wote ambao mmechangia na kuhakikisha tunakutana mahali hapa kuja kushuhudia uzinduzi wa uwanja huu. Niwaombe wanaSingida, uwanja huu ni wa kwenu, mna wajibu wa kuutunza na kuhakikisha kuwa miundombinu hii inabaki hivi hivi kwa kutambua kuwa mkoa huu ni mahali panapotajwa kuwa na mazingira mazuri ya kuchezesha NBC Premiere League pamoja na michezo mbalimbali,” alisema Mwinjuma.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Airtel Tanzania, Franky Filman, alisema kuwa uamuzi wa Airtel Tanzania kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa uwanja huo umeonyesha dhamira ya dhati ya kampuni hiyo kukuza mchezo wa mpira wa miguu na kuwasaidia vijana kupata fursa katika sekta mbalimbali, zikiwemo michezo na burudani.
“Uwanja wa Airtel utakuwa sehemu muhimu ya kulea vipaji vya mpira wa miguu, ukiwapa wachezaji chipukizi jukwaa la kuonyesha uwezo wao na kufanikisha ndoto zao za kuwa nyota wa mpira wa miguu. Mbali na mpira wa miguu, uwanja huu utatumika kwa mashindano mbalimbali ya michezo, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuhakikisha miundombinu hii inatumika kwa muda mrefu,” alisema.
Filman aliongeza kuwa, “Michezo daima imekuwa nyenzo yenye nguvu ya kuunganisha jamii. Katika historia, michezo kama soka imeweza kuvuka mipaka ya kikabila, lugha, na jiografia, ikiwaleta watu pamoja kwa mshikamano na kuwajengea hamasa kwa pamoja. Katika viwanja kama hiki, mashabiki wanakaa bega kwa bega, wakifurahia mchezo wanaoupenda kwa moyo wa ushindani wa kirafiki. kukamilika kwa uwanja huu kutaongeza fursa za ajira kwa vijana, wakiwemo mawakala wa Airtel Money na wauzaji wa bidhaa za Airtel, kuhakikisha mashabiki wanapata huduma bora kabla, wakati na baada ya mechi.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Makete, Festo Sanga alisema kuwa uwanja huo umejengwa kwa ushirikiano kutoka kwa wadau kama vile Airtel Tanzania pamoja na wadau wengine huku akiomba wadhamini wengine wajitokeze na kuunga mkono wadau wa michezo, Singida Black Stars katika ujenzi wa viwanja katika maeneo mengine ambayo yamesalia.
Uwanja huo wa Airtel Stadium ilipambwa na mechi ya kirafiki kati ya mwenyeji Singida Black Stars dhidi ya Yanga SC mechi ambayo hata hivyo ililazimika kuhairishwa katikati ya kipindi cha pili huku matokeo yakiwa ni 1 – 1 kutokana na hali ya mvua kuzidi.