Na Silivia Amandius.
Bukoba, Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, amesikiliza na kushughulikia kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Katoju, Kata ya Bujugo, mnamo Aprili 2, 2025.
Wananchi walilalamikia changamoto kadhaa, ikiwemo ugawaji holela wa ardhi ya kijiji kwa wawekezaji bila kufuata taratibu, utapeli katika mchakato wa kuunganishiwa umeme, kuhamishwa kwa watoto kutoka shule zao bila utaratibu sahihi, pamoja na ucheleweshaji wa malipo ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Akijibu malalamiko hayo, Mhe. Sima alisema tayari amepokea taarifa kuhusu ugawaji wa ardhi kinyume cha sheria na ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kushirikiana na vyombo vingine kufuatilia suala hilo kwa kina.
Kuhusu mwananchi aliyedaiwa shilingi 600,000 na mtu aliyetambulika kuwa mfanyakazi wa TANESCO kwa huduma ya umeme, Mkuu wa Wilaya alieleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua. Aidha, aliwataka mawakala wa huduma vijijini kujiandikisha rasmi katika ofisi za vijiji ili kuepusha utapeli.
Kuhusu malipo ya TASAF, Mhe. Sima alieleza kuwa kupitia mratibu wa mpango huo, fedha za walengwa zitalipwa katika dirisha lijalo la malipo.
Kwa upande wa ardhi, maafisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba walifafanua kuwa ardhi ya kijiji haitauzwa bali hugawiwa kwa wawekezaji kwa masharti ya kuchangia maendeleo ya kijiji. Aidha, mwekezaji asipotekeleza mradi wake ndani ya miaka mitatu, anatakiwa kurudisha eneo hilo kwa serikali ya kijiji.