* Aguswa namna watoto hao wanavyofundishwa stadi za maisha
*Al Muntazir yahudumia zaidi ya wanafunzi 100 wenye mahitaji maalum
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza walimu na uongozi wa Shule ya Al Muntazir kwa kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa upendo mkubwa.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Aprili 6, 2025 katika viwanja vya Shule ya Al Muntazir iliyopo jijini Dar es salaam mara baada ya kufanya matembezi ya Maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani iliyofanyika shuleni hapo kitaifa.
Amesema mara baada ya Mungu kumuumba mwanadamu mtu mwingine anayeweza kumuumba mwanadamu kwa kumfundisha na kumkuuza kimaarifa na maadili ni mwalimu.
“ Tumeona watoto hawa wanafanya kazi mbalimbali, wanafundishwa na wanaongozwa vizuri niwapongeze walimu wote wa shule hii mnaofundisha watoto wenye mahitaji maalum pamoja na uongozi wa shule mmefanya kazi hii kwa watoto kwa ujuzi mlionao mmefanya wanaweza kuimba kuandika, kutengeneza sabuni na vitu mbalimbali,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea “ Tumekusanyika hapa ili kuadhimisha Siku ya Usonji Duniani. Pia kuuambia ulimwengu kuwa tunatambua na kujali kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu. Shule za Al muntazir zimeanza na sisi washiriki tuna wajibu wa kuendeleza na kuienzi azma hii.”
Aidha, uongozi wa shule za Al muntazir ulianzisha shule ya watoto wenye mahitaji maalumu Januari, 2013 na kutoa malezi kwa watoto wenye ugumu katika kujifunza kati ya umri wa miaka 4 hadi 20. Ambapo sasa ina wanafunzi 100 kutoka wanafunzi 39 walikuwepo mwaka 2013.
Vilevile, Dkt. Biteko amesema uongozi wa hiyo unafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa huduma ya namna hiyo inawafikia wadau wengine wa nje.
Ametaja baadhi ya jitihada kuwa ni kuendeleza raslimali watu na nyingine ili kukabiliana na changamoto zilizopo pamoja na kutoa huduma ya mafunzo kwa walimu wa kawaida na wale wa watoto maalum katika maeneo mengine ya Dar es salaam, Arusha na Zanzibar.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema “ Hii ni zaidi ya shule ni tiba kwa vile ndani ya kufundisha wanatibu pia kwa kutumia fursa mbalimbali.”
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar wa salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo amewashukuru walimu wa Shule hiyo kwa kuwatunza watoto hao wenye mahitaji maalum ambao wameendelea kuwasaidia kwa kubuni miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji wa sungura.
Naye, Rais wa Jumuiya ya Khoja Shia Itha Ashar Jamaat, Mohammed Raza Dewji amesema kuwa wanatarajia kujenga kituo cha kisasa kitakachohudumia wanafunzi 500 ambacho kitajumuisha huduma mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi na kusaidia kuongeza ushirikiano wa wanafunzi karibu na jamii ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali katika maisha yao siku za baadae.
“ Hii si ndoto bali ni ushirikiano wa kila mmoja katika jamii kwa kujitoa na kuchangia kwa moyo kwa sababu watoto hawa wanahitaji huduma zaidi,” amesema Dweji.