Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesisitiza umuhimu wa kuangazia maeneo yenye tija kwa maendeleo ya pamoja kati ya Tanzania na Angola, akibainisha kuwa ushirikiano wa kweli lazima ujikite kwenye maeneo yenye fursa halisi za kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.
Akizungumza jijini Luanda, Angola, mbele ya ujumbe wa Tanzania uliowasili kushiriki katika maandalizi ya ziara kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Kombo alisema kuwa ziara hiyo inalenga kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya mataifa haya mawili.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa maeneo tutakayojadili katika ziara hii yanaakisi malengo ya kimaendeleo ya nchi zetu. Tuangalie maeneo yenye tija ya moja kwa moja kwa wananchi wetu,” alisema Mhe. Kombo.
Waziri Kombo aliwahimiza wajumbe kutoka taasisi na wizara mbalimbali za Tanzania kutumia fursa ya maandalizi haya kuchambua kwa kina maeneo yatakayochangia kukuza uchumi, kuongeza ajira, na kuinua maisha ya wananchi kupitia ushirikiano wa kimkakati.
Amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Angola unapaswa kuimarishwa zaidi katika sekta muhimu kama biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, madini, afya, elimu, miundombinu, utalii, mawasiliano, pamoja na masuala ya ulinzi na usalama wa kikanda.
“Ziara hii ya kihistoria ya Rais Samia inatarajiwa kuleta matokeo makubwa, siyo tu kwa upande wa mahusiano ya kidiplomasia, bali pia katika kutafsiri kwa vitendo fursa zilizopo kwa manufaa ya wananchi wetu,” aliongeza Waziri Kombo.
Alisisitiza kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kushirikiana na Angola katika miradi ya pamoja ya maendeleo ambayo itachochea ukuaji wa sekta za kimkakati, kuboresha mifumo ya uchumi na kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.
Ujumbe wa Tanzania ukiwa chini ya uongozi wa Mhe. Waziri Kombo, upo nchini Angola kwa ajili ya maandalizi ya ziara kitaifa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 7 hadi 9 Aprili 2025.