Unguja
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeanza rasmi utekelezaji wa miradi ya amali kwa upande wa Zanzibar, ambapo shilingi bilioni 3.2 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za mafunzo ya amali.
Katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 8 Aprili 2025 kwenye ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) kisiwani Unguja, Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha amesema kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa mamlaka ya kuhakikisha mafanikio ya uboreshaji wa Sera ya Elimu na mtaala mpya unaolenga elimu jumuishi na ya vitendo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu – Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bw. Khalid Waziri, ameshukuru na kuipongeza TEA kwa utekelezaji wa miradi hiyo kwani asilimia kubwa ya shule zilizopo visiwani Zanzibar hazina miundombinu ya amali.
Aidha, Bw. Waziri alifafanua kuwa Wizara ya Elimu imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo, moja ikiwa Unguja na nyingine Pemba ili kuhakikisha kuwa watoto wa Zanzibar wanapata fursa sawa ya elimu.
Kazi ya ujenzi wa shule hizo inatarajiwa kuanza mara moja, huku hatua za awali za usanifu wa michoro, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na maandalizi ya maeneo zikiendelea. Miradi hii itahusisha ujenzi wa shule mbili, ambapo kila shule itakuwa na wastani wa amali tatu zinazotolewa kwa wanafunzi.
Ujenzi wa shule hizi unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu visiwani Zanzibar kwani itatoa fursa kwa vijana wengi kujiendeleza katika fani mbalimbali za amali.
Kupitia miradi hii, Zanzibar itakuwa na fursa ya kuwa na vijana wenye ujuzi wa vitendo watakaoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, na hivyo kuchangia katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

