Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko amesema kuwa pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha uwepo wa upatikanaji wa uhakika wa Nishati ya Umeme,Mafuta na Gesi asilia lakini bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ikiwemo Mabadiliko ya Tabianchi na uharibifu wa Mazingira ambacho ndio kimekuwa kilio kikubwa ndani ya Sekta hiyo.
Dkt Biteko ameyasema hayo Leo Jijini Dodoma Aprili 9,2025 wakati akizindua Taarifa za Maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa mwaka 2023/24.
Na kusema kuwa pamoja na hayo pia upungufu na uchakavu wa miundombinu umeendelea kuwa donda ndugu ambapo sasa wameamua kuanza kufanya marekebisho na ukarabati wa kutosha katika kipindi hiki ambacho kuna umeme wa kutosha.
“Pamoja jitihada kubwa ambazo Serikali imezifanya katika kuhakikisha upatikanaji wa Nishati ya umeme,nishati ya Mafuta na Nishati ya Gesi asilia bado Sekta yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile Mabadiliko Tabianchi na uharifu wa Mazingira kimekuwa kilio kikubwa sana kwenye hii. Ambapo vyanzo vingi maji ambavyo vinatumika kuzalisha umeme mahali pengine vinaharibiwa sana na kufanya changamoto ya upatikanaji wa umeme kuendelea kuwepo”.
Aidha amezitaka Mamlaka zinazohusika na Nishati ya mafuta kuangalia kila namna ya kuhakikisha kuwa bei ya mafuta inakuwa halisi na sio zile zisizoeleweka pamoja na kwamba kumekuwepo na kuimarika kwa upatikanaji wa mafuta Nchini.
“Upatikanaji wa mafuta nchini umeendelea kuimarika sana na ndomana tunaona kuwa biashara ya mafuta hapa nchini imeendelea kuwa ya wazi. Lakini pamoja na hali hiyo bado kuna kazi ya kufanya ili tuangalie kila namna ya kuhakikisha kuwa bei ya mafuta inakuwa halisi na si vinginevyo”.
Awali akitoa neno la Utangulizi Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt James Andilile amesema katika mwaka 2023 walianza na changamoto kidogo katika upatikanaji wa Umeme lakini kutokana na juhudi za Serikali ilipofika mwezi Februari 2025 tatizo hilo lilifika ukomo baada ya kuanza kwa uzalishaji wa umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambapo zilipatikana Megawati 490.
Na kusema kuwa kwa mwaka huo pia miundombinu ya kusafirisha umeme iliongezeka kwa takribani asilimia 9 na pia ujenzi wa Sabustation 4 ulifanyika sambamba na ongezeko la miundombinu ya usambazaji wa umeme kwa asilimia 15.
Akitoa salam za Mkoa wa Dodoma aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe Dkt Sophia Kizigo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa amesema hali ya upatikanaji wa Umeme,Mafuta, Gesi asilia na Nishati kwa ujumla kwa Mkoa huo imeendelea kuimarika na kupanda siku hadi siku.
Ripoti zilizozinduliwa leo ni pamjoa na Ripoti ya Nishtai ya Umeme, Nishati ya Mafuta na Nishati ya Gesi asilia.