Na John Bukuku
Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafiri kwenda Tanzania Bara kwa matibabu ya kibingwa kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya afya visiwani humo.
Akizungumza leo Aprili 11, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Afya Zanzibar (Zanzibar Afya Week 2025), Mazrui alisema kwa sasa wastani wa wagonjwa 200 husafiri kila mwezi kwenda Bara, hali inayogharimu serikali takribani shilingi milioni 400 kila mwezi.
“Zanzibar tuna madaktari 134 tu, na kati yao ni wanne tu waliobobea. Hali hii inalazimu wagonjwa wetu kwenda taasisi kama JKCI na Muhimbili kwa matibabu ya kibingwa,” alisema Mazrui, huku akibainisha kuwa mashirikiano kati ya serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamekuwa msingi muhimu wa kupatikana kwa huduma hizo.
Mazrui alisema kupitia Wiki ya Afya Zanzibar, yenye kaulimbiu ‘Tuanze safari ya mabadiliko kwenye sekta ya afya’, serikali inalenga sio tu kuboresha miundombinu ya afya bali pia kuvutia wawekezaji kwenye huduma za tiba utalii.
“Kwa sasa tunapokea takribani watalii 200 kwa mwezi wanaofika kwa ajili ya huduma kama kujifukiza na kupigwa nyungu, ambazo hulipiwa fedha nyingi. Hii ni fursa ya kiuchumi na ajira kwa vijana,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mangere Miraji, alisema maadhimisho hayo yatashughulikia maeneo manne makuu: kuongeza uelewa wa afya kwa jamii, kutambua mchango wa wadau wa sekta ya afya, kuendeleza utalii wa tiba, na kukuza matumizi ya teknolojia katika huduma za afya.
“Ushirikiano kati ya Zanzibar na Dar es Salaam utasaidia kufikisha huduma bora kwa makundi yenye changamoto za kiafya na kuboresha ushirikiano wa sekta binafsi na za umma,” alisema Dkt. Miraji.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Mohamed Mang’una, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma katika kuimarisha utalii wa afya, huku Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, akibainisha kuwa mkoa uko tayari kushiriki kikamilifu katika mpango huo kwa kuanzisha vikao na mikakati ya pamoja.
Wiki ya Afya Zanzibar inat awarajiwa kufanyika kuanzia Mei 4 hadi Mei 10, 2025, mjini Zanzibar, ikiwa ni hatua ya mwanzo kuelekea mageuzi ya kina katika sekta ya afya ya visiwani humo.