Na Mwandishi Wetu TABORA
WATUMISHI kutoka Taasisi mbalimbali wametakiwa kuzingatia taratibu za manunuzi ili kuepusha mianya ya Rushwa na kuendelea kujenga uchumi wa nchi imara kwa manufaa ya taifa.
Hayo yanesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Matiko Chacha wakati akifunga mafunzo ya kujengea uwezo watumishi kutoka taasisi mbalimbali kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST ambayo yamefanyika kuanzia Aprili 07 hadi 11, 2025 katika ukumbi wa Mwanakiyungi Mkoani Tabora.
Mhe. Paul amesema mafunzo hayo yamekuwa ya kipekee kwa sababu yamejikita katika moduli mpya na muhimu kwa maboresho ya michakato ya ununuzi wa umma nchini ambapo Mfumo wa NeST unaendelea kuboresha uwazi, uwajibikaji, na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.
“Sasa ndugu zangu mara nyingi tunasikia mfumo unachelewesha lakini mimi nasema mifumo haicheleweshi, mifumo hii imekuja kwaajili ya kurahisisha kazi zetu sasa ninyi wataalamu wetu mpo hivyo muikotroo na kwa bahati nzuri mifumo hii inaindeshwa na wewe hivyo tujitahidi kuwa waadilifu ili tuache kusingizia mfumo”alisema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhandisi Deusdetith Katwale amesema mafunzo hayo ni muuendelezo wa jitihada za serikali katika kuhakikisha changamoto za ununuzi ndani ya taifa ziwe zinashughulikiwa kimifumo ili kuendana na teknolojia inayozidi kushika kasi nchini.
“Sasa hivi serikali inashika kasi kwenye mambo ya kidijitali ambapo zamani tulikuwa tunasema serikali inawasiliana kwa makaratasi tu lakini sasa hivi serikali tunawasiliana kidijitali kwa hiyo ni mwendelezo wa kuhakikisha inakuwa na mifumo imara ya mawasiliano hivyo ni imani yangu kwamba mafunzo yaliyofanyika hapa yataendelea kuleta chachu na kupunguza mianya ya rushwa katika Serikali yetu” aliongeza Mkuu wa Wilaya.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri kutoka PPRA Makao Makuu, Bi. Winfrida Samba amesema, lengo kuu la mafunzo hayo ni kupata elimu kuhusu Mfumo wa NeST na katika mfumo huo kuna moduli mbalimbali na nyingine ni moduli ni mpya ambazo zilizopelekea kufanya mafunzo hayo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa katika Mfumo wetu wa NeST tuna moduli mbalimbali ikiwemo usajili ambayo inahusika na wazabuni pamoja na taasisi nunuzi, moduli nyingine ni “Etendering” ambayo inahusika na uchakataji wa zabuni pia tuna moduli ya “E-contract Management” ambayo nayo inahusika na usimamizi na utekelezaji wa Mikataba, tuna “Epayment”ambayo inahusika na masuala ya malipo lakini pia tuna moduli ndogo ambazo hizi ndizo washiriki wamejifunza zaidi” alisema Mkurugenzi Samba.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa serikali kuhusu Mfumo wa NeST yameanza tarehe 7 hadi 11 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Mwanakiyungi Mkoani Tabora.