Na Silivia Amandius,
Kagera.
Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na waratibu wa Kampeini ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC), imetoa mafunzo maalum ya mwongozo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera watakaojitokeza kuwasilisha changamoto zao zinazohitaji msaada wa kisheria.
Mafunzo hayo yamewanufaisha wataalamu mbalimbali wakiwemo maofisa ustawi wa jamii, maofisa maendeleo ya jamii, maofisa ardhi, mawakili wa kujitegemea, maofisa kutoka madawati ya kijamii ya polisi, watendaji wa kata zitakazotembelewa pamoja na wanasheria kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Kagera.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Kampeini ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Bi. Ester Msambazi, alisema kampeini hiyo imeleta mafanikio makubwa tangu ilipoanzishwa mwezi Mei 2023. Mafanikio hayo ni pamoja na utatuzi wa migogoro ya muda mrefu, kuimarika kwa mawasiliano kati ya wananchi na watoa huduma za kisheria, na kuongeza uelewa wa wananchi juu ya haki zao za kisheria.
“Tunapotoka hapa baada ya kupatiwa mafunzo, ni muhimu tuweke pembeni vyeo vyetu, tushirikiane kama timu moja, tufanye kazi kwa weledi na kuwa wasikivu kwa wananchi. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata msaada wa kutosha na kuendeleza matumaini kwa wale waliokata tamaa kutokana na changamoto za kisheria,” alisema Bi. Msambazi.
Aidha, alibainisha kuwa kampeini hiyo inatarajiwa kutamatika mwishoni mwa Mei mwaka huu, na mara baada ya hapo, kliniki za kutoa huduma za kisheria bure zitafunguliwa katika halmashauri zote. Mwananchi ambaye kesi yake haitatatuliwa ndani ya siku tisa, atapewa wakili wa kumwakilisha hadi kesi hiyo itakapokamilika.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Issaya Tendega alisema Mkoa wa Kagera unakumbwa na changamoto nyingi za kisheria hasa katika maeneo ya migogoro ya ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia, hivyo msaada wa kisheria ni muhimu sana kwa wananchi.
“Tunaomba huduma hizi ziwafikie pia wananchi wa pembezoni, ambao mara nyingi hukosa uwezo wa kugharamia kesi zao. Kupitia kampeini hii, tunaamini migogoro mingi itapungua na wananchi wetu wataongeza imani katika mfumo wa haki,” alisema Bw. Tendega.