Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeitaka jamii kutumia fursa na rasilimali zilizopo katika maeneo yao ili kuleta maendeleo endelevu kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla, sambamba na kuhakikisha hawaanzishi migogoro isiyo ya lazima.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Wakili Amon Mpanju, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Amsha Ari yenye lengo la kuleta mageuzi ya kifikra na mtazamo, ili kuwafanya wananchi kutambua umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Katika hotuba yake, Wakili Mpanju amesisitiza umuhimu wa jamii kuepuka kuanzisha migogoro na badala yake kujikita katika kuitatua ili kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani yasiyo na tija. Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano wanapohitajika, hususan wanapopeleka mashauri mahakamani.
> “Tujikite kwenye kuwekeza katika kuzuia migogoro. Tukifanya hivyo, hatutaiona mahakama. Lakini pale ambapo shauri limepelekwa mahakamani, semeni ukweli kama mtu amefanya makosa,” alisema Wakili Amon Mpanju, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum.