Wajumbe wa Kamati ya Wanawake Chavita Taifa pamoja na wadau wengine wakiwa kwenye picha ya pamoja muda mfupi mkoani Morogoro jana baada ya kumaliza kikao cha uchechemuzi na ukusanyaji maoni kuhusu mkataba wa Itifaki ya masuala ya Ulemavu ya Afrika, unaotarajiwa kupelekwa bungeni hivi karibuni kwa hatua za uidhinishaji.
……………………………………….
Na Godwin Myovela, Morogoro
CHAMA cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), kupitia kamati yake ya wanawake taifa kimemuomba Rais Samia kufanikisha mchakato wa utiaji saini wa mkataba wa Itifaki ya masuala ya Ulemavu ya Afrika, ili kuboresha ubora wa maisha na kuchochea upatikanaji wa fursa mbalimbali.
Wakizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo kitaifa mkoani hapa jana, mwenyekiti wa kamati ya wanawake chavita, Tatu Kondo, alisema anamsihi Rais Samia aungane na mataifa hayo mengine kusaini itifaki hiyo yenye lengo la kulinda na kukuza haki za watu wenye ulemavu barani Afrika.
Alisema anatamani kuona walemavu wakishirikishwa ipasavyo katika kuchangia kuunda sera na mifumo jumuishi inayowaakisi, sambamba na utatuzi wa changamoto sugu ya ukosefu wa mawasiliano kwenye shughuli zote za kijamii kunakosababishwa na utambuzi finyu wa lugha ya alama na wakalimani-hali inayodumaza maendeleo yao.
Hata hivyo, mratibu wa kamati hiyo, Lupy Mwaisaka alisema azma ya kikao hicho ni kukusanya maoni na kufanya uchechemuzi juu ya mkataba wa itifaki hiyo unaosisitiza zaidi misingi ya kuheshimu haki za wenye ulemavu, usawa na ukuzaji wa sera jumuishi, hasa uboreshaji na utambuzi wa lugha ya alama kabla ya kufikisha mapema kwenye bunge linaloendelea
Imeelezwa kwamba ili kuanza kutekelezwa kwa mkataba huo ni sharti kuanzia nchi 15 ziidhinishe kwa kuweka amana. Hadi sasa Tanzania haijaridhia tangu kuanza kwa uidhinishaji wa mataifa mbalimbali kwa kipindi cha miaka 27 mpaka sasa.
Hadi kufikia 29 Novemba 2023 ni mataifa 12 pekee yakiwemo Angola, Burundi, Cameroon, Kenya, Mali, Msumbiji, Namibia, Niger, Rwanda, Sahrawi Arab Democratic Republic, Afrika Kusini, na Uganda ndiyo yaliyoidhinisha
Aidha, Kondo alisema endapo mkataba huo utasainiwa utaongeza ufahamu kuhusu Itifaki ya masuala ya Ulemavu ya Afrika (African Disability Protocol) na kuelimisha umma na watunga sera juu ya umuhimu wa uidhinishaji wake, na kusaidia kujenga usaidizi mpana.
“Tunatambua mchango wa Rais katika kushughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu, tunampongeza kwa yote, na kwenye ombi letu hili tunamsihi Tanzania isaini kabla ya Bunge kumalizika ili kuunda jamii inayojumuisha zaidi, hususan kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema
Aidha, katika kikao hicho kilichoratibiwa na chavita taifa, chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa la ADD, wadau hao wamehimiza jamii kuachana na mila potofu, kandamizi na ubaguzi uliokithiri dhidi ya watu wenye ulemavu, na badala yake kuzingatia upendo na ushirikiano kwa maslahi mapana ya taifa.
Makamu Mwenyekiti wa Shiviwata, Tungi Mwanjala alisema “mathalani hivi sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu…nivisihi vyama vya siasa kuweka mifumo rafiki ya kutuwezesha kushiriki chaguzi, lakini pia serikali ihamasishe wenye ulemavu kujitokeza kugombea.” .
Wajumbe wa Kamati ya Wanawake Chavita Taifa pamoja na wadau wengine wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Wajumbe wa Kamati ya Wanawake Chavita Taifa pamoja na wadau wengine wakiwa kwenye picha ya pamoja.