Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa wito kwa wataalamu wa sekta mbalimbali kuwa na utamaduni wa kuwashirikisha wananchi pamoja na wadau wa maendeleo kabla ya kufanya maamuzi muhimu yanayohusu ustawi wa jamii.
Akizungumza tarehe 14 Aprili 2025 wakati wa ziara yake katika Manispaa ya Songea, Kanali Ahmed alieleza kuwa ushirikishwaji wa jamii kupitia vikao na mikutano ni nguzo muhimu katika kuhakikisha maamuzi yanayochukuliwa yanaendana na mahitaji halisi ya wananchi.
Katika ziara hiyo, alitembelea maeneo ya Stendi ya Ruhuwiko na Mfaranyaki, ambako alisikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wananchi na wafanyabiashara. Alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi, ikiwemo mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 145, ujenzi wa barabara ya mchepuko (Bypass) ya Songea, pamoja na ujenzi wa masoko mawili katika eneo la Manzese.
Kanali Ahmed alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, ikiwemo msongamano wa magari makubwa katikati ya mji wa Songea. Alifafanua kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mchepuko zimeshapokelewa, na maandalizi ya kuanza ujenzi huo yanaendelea vizuri.
Kuhusu usalama wa waendesha bodaboda na bajaji, Mkuu wa Mkoa alieleza umuhimu wa kuwa na sare maalum kwa ajili ya utambulisho. Alisema sare hizo zitasaidia kuwatambua madereva hao kirahisi pindi wanapokumbana na matatizo au wanapokuwa kazini. Hadi sasa, sare 300 za kuakisi mwanga tayari zimepatikana kwa ajili ya kuanza kugawiwa kwa madereva hao.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano, alieleza kuwa Serikali imetekeleza agizo la Rais kwa kutenga eneo maalum kwa ajili ya Wamachinga katika eneo la Majengo. Hata hivyo, baadhi ya Wamachinga bado hawajaanza kulitumia eneo hilo kama ilivyokusudiwa.
Meya huyo pia alitoa wito kwa wananchi kuwa na subira wakati Serikali inajiandaa kuanza rasmi ujenzi wa soko la Manzese, ambao maandalizi yake yamekamilika na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza muda wowote kutoka sasa.
Wafanyabiashara walioshiriki katika ziara hiyo waliwapongeza viongozi kwa kuwatembelea na kusikiliza kero zao. Walieleza matumaini yao kuwa changamoto walizowasilisha zitapatiwa suluhisho kupitia juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali.