Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya, ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kupokelewa tarehe 15 Mei 2025.
Akizungumza na wananchi wa kata za Lusewa, Mkongo na Msindo alipotembelea maeneo hayo Malenya alisisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru ni tukio muhimu la kitaifa linalolenga kuhamasisha maendeleo, kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kukuza uzalendo miongoni mwa Watanzania.
“Ni muhimu wananchi wote wakajitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru. Huu ni mwenge unaomulika maendeleo ya taifa letu, na ni fursa ya kuonesha mshikamano, uzalendo na dhamira ya kushiriki katika ujenzi wa taifa,”.
Aidha, alieleza kuwa kupitia mwenge huu, miradi mbalimbali ya maendeleo itazinduliwa na kukaguliwa, hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi hiyo.
Malenya alihitimisha kwa kuwataka viongozi wa mitaa na vijiji kushirikiana kikamilifu katika maandalizi ya mapokezi hayo, kuhakikisha usalama na mshikamano unazingatiwa ili kufanikisha tukio hilo muhimu kwa mafanikio makubwa.
Mwenge wa Uhuru mwaka huu unatarajiwa kuwasili Wilayani Namtumbo mnamo tarehe 15 Mei 2025, na tayari maandalizi mbalimbali yameanza kufanyika kuhakikisha mapokezi yake yanakuwa ya kihistoria.