Mwenyekiti wa Bodi ya Uwekezaji na Fedha ya Watumishi Housing Investment (WHI) Celestine Muganga akitoa maelekezo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Sephania Solomon wakati kamati ya bodi hiyo ilipotembelea mradi wa 101 Mikocheni Apartment.
Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Yusuph Mlimakifu akitoa maelezo kwa kamati ya bodi hiyo wakati ilipotembelea mradi wa 101 Mikocheni Apartment Mikocheni jijini Dar es Salaam
BODI ya Uwekezaji na Fedha ya Watumishi Housing Investment (WHI) ,imetembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba 101 unaotekelezwa katika eneo la Mikocheni, mkoani Dar es Salaam, ambapo ujenzi huo unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 18 hadi kukamilika kwake.
Katika ziara hiyo iliyofanyika jana, wajumbe wa bodi hiyo walionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na viwango vya ubora vinavyotumika katika ujenzi, wakisema ni mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa sera ya makazi bora kwa watumishi wa umma.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Bodi, Celestine Muganga, alisema mradi huo umejengwa kwa ajili ya kusaidia watumishi wa umma na tayari nyumba zote zimekwishalipiwa.
“Tunatambua kuwa mahitaji ya makazi ni makubwa. Tayari eneo hili limekwishalipiwa lote. Tumejionea utekelezaji wenye tija unaoendana na malengo ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha watumishi na wananchi wanapata makazi bora na salama,” alisema Muganga.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Sephania Solomon, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 26, 2026 hukulikiwa ni kuondoa changamoto ya makazi, hususan kwa watumishi wa umma wa kipato cha kati na cha chini.
“Nyumba hizi zimebuniwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, mazingira rafiki na bei nafuu. Tumeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha ili kuwawezesha wanunuzi kupata mikopo kwa masharti nafuu, hivyo kuwasaidia kumiliki makazi yao kwa urahisi zaidi,” alisema Solomon.
Naye Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Yusuph Mlimakifu, alisema ujenzi huo unaohusisha nyumba zenye chumba kimoja, viwili na vitatu umefikia asilimia 20. Alieleza kuwa hadi sasa hakuna changamoto kubwa na wanaendelea na kazi kwa kasi ili kukamilisha mradi kwa wakati kama walivyopanga.
Watumishi Housing Investment imeendelea kutekeleza miradi ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila mtanzania anapata haki ya msingi ya makazi bora.