Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa jiji hilo limejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu, huku Serikali ikiendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa wakazi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama jijini, Chalamila amesema kuwa hakuna atakayeruhusiwa kuvuruga amani iliyojengwa kwa juhudi kubwa kwa kipindi kirefu, na kwamba vyombo vya dola vinaendelea kuhakikisha hali hiyo inadumu.
“Hali ya nchi yetu kwa sasa ni shwari kama alivyoeleza Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, na tunaendelea kuimarisha ulinzi hasa katika kipindi hiki tunapokaribia uchaguzi,” amesema Chalamila.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewatoa hofu wafanyabiashara wanaojishughulisha na shughuli za usiku akisema mpango wa biashara masaa 24 unaendelea vizuri na hakuna tishio lolote kwa usalama wao.
Pia amewahimiza wananchi kupuuza jumbe za uchochezi zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii na kuendelea kushiriki katika shughuli zao za kila siku kwa utulivu.
Aidha, Chalamila amewatakia Wakristo maandalizi mema ya Sikukuu ya Pasaka, akiwataka kusherehekea kwa amani kama ilivyoshuhudiwa wakati wa sikukuu za Idd zilizopita.