Na Janeth Raphael MichuziTv
MBUNIFU na Mkurugenzi wa Kampuni ya Nunu get software Development Company Jeremiah Malamka ameipongeza serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),Kwa kufanikisha kuwawezesha wabunifu kupata mikopo nafuu.
Malamka ambaye ni mnufaika wa mikopo hiyo,amesema hatua hiyo imefuta dhana ya muda mrefu ya “Poor Government Support” na ukosefu wa fedha, ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ikitajwa kwenye vitabu vya taaluma.
“Tumeisoma ‘Poor Government Support’ kwenye vitabu miaka mingi, lakini sasa tumeishuhudia historia ikiandikwa,”amesema Malamka.
Amesema Serikali imeonyesha kwa vitendo kuwa ipo tayari kusimama na wabunifu wake hivyo nao wataendelea kupambana ilinkuhakikisha wanatumia fursa zinazotolewa na serikali.
Aidha, Malamka ameishukuru COSTECH kwa hatua ya kuwatambua wabunifu wa Kitanzania na kuwapa hadhi inayostahili, akisema hatua hiyo si tu imewapa heshima, bali pia imewapa nguvu mpya ya kuamini kuwa wanathaminiwa na taifa lao.
“Kwa miaka mingi wabunifu tulikuwa kama watu walioachwa nyuma. Leo COSTECH imetufanya tuhisi kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa maendeleo. Tunawashukuru sana kwa kututambua,” amesema.
Mpango huu wa ushirikiano kati ya COSTECH na CRDB unalenga kutoa mikopo nafuu ya jumla ya Shilingi Bilioni 4.6, ambapo kati ya hizo, Serikali kupitia COSTECH imetoa dhamana ya Bilioni 2.3.
Hii ni hatua ya utekelezaji wa moja kwa moja wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha vijana na kukuza uchumi wa viwanda kupitia ubunifu wa ndani.
Mbali na hayo, aliwahimiza wadau wengine kutoka sekta binafsi, mashirika ya maendeleo, na serikali za mitaa kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha kuwa kila wazo la ubunifu linapewa nafasi ya kukua na kuwa chanzo cha ajira, mapato, na heshima ya kitaifa.