
Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT

Na Khadija Kalili, Michuzi TV
MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba nane za kulala wageni zinazojengwa katika bustani ya wanyama ambayo inasimamiwa na kikosi cha Jeshi 832 Ruvu JKT Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Meja Jenerali Mabele amesema sababu ya kuanzishwa bustani za wanyama kwenye vikosi ni pamoja na kuongeza vyanzo vya mapato na kutangaza utalii hapa nchini.
Meja Jenerali Mabele amesema mradi wa bustani ya wanyama mbali ya kuwepo katika Kikosi hicho pia mradi kama huo upo Kikosi cha Mbweni Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa bustani hiyo ni sehemu ya kutangaza utalii na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour na kwamba JKT Ruvu wataendelea kuongeza wanyama ili kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Mkuu huyo wa JKT amesema uwepo wa bustani hiyo unawawezesha wananchi wanaoshindwa kwenda katika mbuga za Mikumi na nyingine hapa nchini kujionea wanyama mbalimbali katika eneo hilo.
“Tutaendelea kuongeza wanyama rafiki katika hii bustani ya wanyama na nyumba hizi za kulala zitawawezesha sasa wanaopata fursa ya kutembelea hapa kupata mapumziko kufurahia utalii wa ndani huku wakipata huduma zote hapa,” amesema Meja Jenerali Mabele.
Kamanda wa Kikosi cha Ruvu JKT Kanali Peter Mnyani amesema vijana wanaopatiwa mafunzo katika kikosi hicho wamekuwa wakipata mafunzo kwa vitendo na kujifunza uzalendo na shughuli za kiuchumi.
Mbali ya kuweka jiwe la Msingi Meja Jenerali Rajabu Mabele amefunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea Operesheni Miaka 60 ya muungano katika Kikosi cha Jeshi 832 Ruvu JKT.