TAARIFA RASMI KUTOKA CHAMA CHA NLD APRILI 18, 2025,
CHAMA cha National League for Democracy (NLD) kinapenda kuwataarifu wanachama, wafuasi na wananchi kwa ujumla kuwa, kufuatia Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika tarehe 10 Aprili 2025, wajumbe wa mkutano huo kwa kauli moja waliridhia mapendekezo ya kubadilisha bendera na nembo ya chama.
Mabadiliko haya ni ya heshima na kihistoria, yakilenga kusawiri kwa undani zaidi maono, dira, na mwelekeo mpya wa chama chetu kuelekea kujenga taifa lenye demokrasia imara, usawa wa kijamii, Uzalendo Haki na Maendeleo.
Kupitia uongozi imara wa Mwenyekiti wa Taifa Mhe. Khamis Mfaume na Katibu Mkuu Doyo Hassan Doyo, Sekretarieti ya chama imekamilisha maboresho ya nembo na bendera mpya, ambazo sasa zinakwenda kutambulika rasmi kitaifa na kimataifa kama utambulisho wa chama.
RANGI YA BENDERA MPYA YA NLD NA MAANA YAKE.
Njano, Inaashiria maliasili, misitu na madini.
Nyeusi, Ni alama ya utu wetu, asili yetu na uafrika wetu.
Bluu, Inawakilisha rasilimali za maji, bahari, mito na maziwa (Blue Economy).
Nyekundu, Inawakilisha harakati za mapambano ya demokrasia katika nchi yetu.
NEMBO MPYA YA NLD.
Mkono mmoja wa ushindi (Victoria), unaashiria matumaini, nguvu na mafanikio.
Nyota tatu, zinawakilisha dira isiyo na kikomo ya chama chetu.
Kwa niaba ya uongozi wa chama, tunawapongeza sana wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa uamuzi huu wa busara na kizalendo. Mabadiliko haya yanadhihirisha kukua kwa chama na dhamira ya chama kusimamia misingi ya demokrasia, utawala bora na mshikamano wa kitaifa.
#NLD #MageuziYaKihistoria #DemokrasiaKwaVitendo #BenderaMpyaNLD #NemboMpyaNLD
NLD: Ukombozi wa Umma.
NLD: Mtetezi wa Umma.
NLD: Moto Moto Motooo!
Imetolewa na: Idara ya Habari na Mawasiliano
Chama cha NLD
Tandika, Temeke Jijini Dar es salaam, Tanzania
Tarehe: 18 Aprili 2025