Baadhi ya Wakulima wa kahawa katika kijiji cha Nyoni Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Afisa Ushirika wa Halmashauri hiyo Nuhu Serenge kushoto kuhusu umuhimu wa kufuatilia uzalishaji wa kahawa ili kupata kahawa bora itakayokuwa na soko la uhakika kwenye minada.
Baadhi ya Wakulima wa kahawa katika kijiji cha Nyoni Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma wakiondoa majani yasiyohitajika kwenye kahawa ili kupata kahawa yenye ubora,katika msimu wa kilimo 2024/2025 zaidi ya tani 326 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,049,369.350. zilikusanywa na kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
……..
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
WAKULIMA wanaojihusisha na kilimo cha zao la kahawa katika kijiji cha Nyoni kata ya Nyoni Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wamesema,mbolea za ruzuku walizopewa na Serikali kwa gharama nafuu zimesaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Wameeleza kuwa, mbolea hizo zimehamasisha watu wengi hususani vijana wa kata ya Nyoni kujikita kwenye kilimo cha zao la kahawa ambalo limepunguza tatizo kubwa la umaskini kwa watu wengi na kuachana na kilimo cha mazao mengine kama mahindi ambayo yanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo bei ndogo na gharama kubwa za uzalishaji wake.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Nyoni Thobias Nzuyu alisema,awali pembejeo za kilimo hasa mbolea walizipata kwa shida na wakati mwingine walilazimika kwenda kununua Wilayani Songea,hivyo kusababisha baadhi ya wakulima kukata tamaa na wengine kususia mashamba yao.
“Kabla ya kuanza mpango wa mbolea za ruzuku, nimewahi kwenda Wilaya jirani ya Songea na kukaa uko zaidi ya wiki mbili ili kupata mbolea kwa ajili ya wakulima wangu,lakini Serikali ilivyoleta mpango huu kwa kweli umesaidia sana kuwarudisha wakulima wengi mashambani,tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia kwa kututhamini sisi wakulima”alisema Nzuyu.
Nzuyu alisema,sasa Vyama vya Msingi vya Ushirika(Amcos) ndiyo vina jukumu la kukusanya kahawa za wakulima na kutafuta soko la pamoja na kuziuza kwa kufuata mfumo wa stakabadhi mazao ghalani ambao umeleta tija kubwa kwa vyama na wakulima.
Pia alisema,katika kipindi cha miaka minne cha Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,bei ya kahawa imeongezeka kutoka Sh.3,500 msimu wa kilimo 2021/2022 hadi kufikia Sh. 8,667 kwa kilo moja.
Ameiomba Serikali, iendelee na mpango wake wa kutoa ruzuku kwenye mbolea kwani utasaidia wakulima kulima kwa tija na kupata mafanikio makubwa kupitia shughuli zao za kilimo.
Katibu wa Chama hicho Hyasint Nzuyu alisema,takwimu zinaonyesha mavuno yameongezeka kutokana na huduma wanazopata kutoka Serikalini kuwa za uhakika ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo wakulima walijitegemea kutafuta pembejeo na mahitaji yao mengine kwa ajili ya shughuli zao za kilimo.
Ametaja baadhi ya huduma wanazopata ni mikopo ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo ikiwemo mbolea na madawa ya kuuwa wadudu na magonjwa ya kahawa, huduma za ugani na elimu ya Ushirika.
Alieleza kuwa,katika msimu wa kilimo 2023/2024 walikusanya jumla ya tani 441 na msimu 2024/2025 wamefanikiwa kukusanya tani 326 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,049,369.350.
Ameishukuru Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma ambayo msimu wa kilimo 2023/2024 iliidhinisha Sh.milioni 500 kati ya hizo Sh.milioni 150 ili kununua pembejeo na Sh.milioni 350 kwa ajili ya malipo ya awali kwa wakulima.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa inayowasumbua ni kucheleweshwa kwa mikopo ya pembejeo na fedha ya malipo ya awali kwa kuwa pembejeo ni muhimu katika uzalishaji kwani bila pembejeo kufika kwa wakati uzalishaji utapungua.
Amesisitiza kuwa,wakulima wakipati fedha za awali watakuwa na uhakika wa kuchuma na kuhudumia mashamba yao na iwapo zitachelewa husababisha kuuza kahawa nje ya utaratibu wa stakabadhi mazao ghalani ili kupata fedha.
Mkulima wa kahawa Ditrick Tilia alisema,katika kipindi cha miaka minne wamekuwa kwenye mafanikio makubwa ikiwemo kahawa kuuzwa kwa bei nzuri na kuongezeka kwa uzalishaji mashambani.
Alisema,miaka ya nyuma bei ya kahawa ilikuwa ndogo isiyolingani na gharama halisi ya uzalishaji,lakini waliendelea kulima zao hilo kwa sababu ya kukosa mazao mengine ya biashara yanayowaingizia kipato.
“naiomba sana Serikali, iwadhibiti wafanyabiashara na wanaonunua kahawa mashambani kwa kutumia vipimo haramu vya magoma kwa bei ndogo,tabia hii inaturudisha nyuma wakulima kiuchumi na inachangia kukosekana kwa takwimu sahihi za uzalishaji wa kahawa,Serikali isimamie sana jambo hili kwa kuwa Vyama vya Ushirika vitanufaika na wakulima watapata faida kubwa”alisema Tilia.
Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Nuhu Serenge alisema,kwenye zao la kahawa Halmashauri inatoa mchango mkubwa ili kuhakikisha wakulima wanapata tija kupitia shughuli zao ikiwemo kutoa elimu namna gani zao la kahawa linavyozalishwa kupitia maafisa ugani.
Alisema,awali ilikuwa vigumu kuwafikia wakulima kwenye maeneo yao lakini,Serikali imetoa Pikipiki kwa kila Afisa Ugani ili aweze kuwafikia wakulima kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutoa huduma za ugani.
Alisema,Halmashauri ya Wilaya inatoa bure mbegu na miche kwa wakulima ili waweze kupanua mashamba yao na kuwaunganisha na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi ya kuboresha zao la kahawa kama vile Kampuni ya AVIV LTD, SoRIDALIDAD na HRNS.
Kwa mujibu wa Serenge ni kwamba, wanaamini kupitia mbolea za ruzuku wakulima wataweza kuzalisha kahawa kwa wingi hali zao za maisha kuwa nzuri na Serikali kupata fedha kutokana na ushuru.