Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere John Baytani
Mwakilishi wa wahitimu wa mafunzo hayo ya vijana Father John Mtwale kutoka Jimbo Katoliki la Mwanza
Na Khadija Kalili ,Kibaha
MKUU wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda amewataka Wakuu wa Idara na Taasisi mbalimbali nchini kutumia Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kuwapa mafunzo na elimu ya Uongozi ya uwajibikaji watumishi wao ili kuondokana na changamoto za migogoro kazini.
Akizungumza mara baada ya kufunga mafunzo ya uongozi Kwa viongozi kutoka Taasisi mbalimbali hapa nchini katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha Kwa Mfipa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda akiwa Mgeni Rasmi amesema shule hiyo ina miundo mbinu bora na elimu inayotolewa ni msaada mkubwa kwa watumishi na wafanyakazi nchini.
Amesema kuna changamoto baina ya wafanyakazi hutokea kwasababu ya matatizo yanayotokana na ukosefu elimu ya uongozi ya uwajibikaji kazini hivyo wanapopata mafunzo hayo kila mmoja hujitambua na migogoro kazini inakwisha.
“Kwa zile Taasisi za Halmashauri na Wilaya zote nchini kada za waalimu waalimu wa taaluma na maadili wote nawashauri waje wapate elimu ya mafunzo ya uongozi katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere ili waweze kuongeza wigo wa elimu zao hata kama tayari wako maofisini kwani elimu haina mwisho” amesema Mapunda.
Amesema kuwa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere ziba ombwe la changamoto elimu ya uongozi kwa viongozi kazini katika nyanja za kada zote nchini hivyo taasisi na idara mbalimbali za serikali na binafsi zitumie kuendeleza watumishi wao.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere John Baytani amesema mafunzo hayo kwa viongozi hao yametolewa kwa kuzingatia ubora pia wamejifunza mambo mbalimbali ikiwamo afya ya akili na namna ya kuongoza rasilimali watu ambapo wametoka wakiwa wameiva.
Baytani amesema wahitimu hao 21 ambao wamepatiwa mafunzo ya uongozi ni vijana kutoka Taasisi mbalimbali nchini na mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa wengine kuona namna ya kujipanga kwenda kujifunza na kupata elimu hiyo ya uongozi shuleni hapo.
Naye mwakilishi wa walihitimu wa mafunzo hayo ya vijana father John Mtwale kutoka Jimbo Katoliki la Mwanza amesema wakitoka hapo wataenda kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata hasa kwa kuwa na mshikamano thabiti.
Father Mtwale amesema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea ufahamu wa uongozi na yamewafungua na kuwapa mbinu kama viongozi za kutawala hisia pindi wanapokuwa na ghadhabu kama binadamu huku amewaomba viongozi wa dini zote pindi watakapopata fursa wakasome shuleni hapo na matunda yake watayaona.
Aidha Father Mtwale amesisitiza viongozi wa dini wote wajitokeze kwenda kupata mafunzo haya yapo hayana mipaka yanasaidia kuibadilisha jamii nzima viongozi wote tuungane katika kuleta mabadiliko ya kweli na siyo kwa viongozi wa dini pekee.
“tumejifunza namna ya kutawala hisia na kuwa watulivu hivi sasa dunia imekumbwa na matatizo ya kupata mfadhaiko na sonona yamekithiri duniani kote,hivyo ukiwa kiongozi changamoto zipo ila ufundi wa kiongozi ni kuzivuka na kuzikabili changamoto hizo” amesema Father Mtwale.