Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma pamoja na Mwakilishi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama na Viongozi mbalimbali mara baada ya kukabidhiwa nakala 3 za Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha Sheria ya urekebu wa sheria kwa ajili ya kumbukumbu, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya uzinduzi wa toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa toleo la Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa toleo la sheria zilizofanyiwa urekebishaji ikulu Chamwino jijini Dodoma.
……………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebishaji la mwaka 2023 katika hafla iliyofanyika leo April 23, 2025 Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema toleo hilo jipya litasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kisheria, kupunguza muda wa utafiti wa sheria, na kusaidia watendaji kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
“Kwa kuwa sheria ni kioo cha ustarabu wa Taifa, ni muhimu ziwe wazi, zinazofahamika na zinazoendana na wakati. hii ni njia ya kuhakikisha haki inapatikana, na raia wanalindwa ipasavyo,” amesems Rais Dkt. Samia.
Aidha, ameeleza kuwa uwepo wa sheria zilizorekebishwa na kupatikana kwa urahisi utapunguza mianya ya matumizi mabaya ya madaraka, kushusha viwango vya rushwa, na kuongeza imani kwa wafanyabiashara na wawekezaji – jambo ambalo litachochea zaidi shughuli za kiuchumi nchini.
Rais Samia amesisitiza kuwa mradi huo wa urekebishaji wa Sheria ni hatua muhimu kwa maendeleo ya Taifa, na utaboresha utendaji wa kazi kwa Taifa.
“Kwa mara nyingi wananchi wamekuwa wakifanya makosa kwa kisingizio cha kutokujua sheria, sasa sheria zinapokuwa wazi na rahisi kupatikana, kisingizio hicho hakitakuwapo tena,” amesema
Katika hotuba yake, amebainisha kuwa zoezi la urekebishaji wa sheria linakwenda kutatua changamoto zilizopo na linatarajiwa kuongeza ufanisi katika nyanja mbalimbali.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa toleo la sheria zilizofanyiwa urekebishaji ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake katika kufanikisha mradi wa Toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebu 2023, hatua inayotajwa kuimarisha matumizi ya sheria, haki na utawala bora nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bw. Johari amesema kuwa urekebu huo ni wa kihistoria na utaanza kutumika rasmi Julai 1, 2025.
Mhe. Johari amesema kuwa urekebu huo umejumuisha marekebisho ya sheria mbalimbali tangu mwaka 2002, pamoja na kuondoa makosa ya uchapaji, kuweka sheria katika mfumo unaoeleweka kwa urahisi.
Ameeleza kuwa toleo hilo lina jumla ya juzuu 21 za sheria kuu pamoja na sheria mpya 171 zilizotungwa kati ya mwaka 2002 hadi 2023, kazi iliyochukua takribani miaka minne kuikamilisha kwa kutumia rasilimali za ndani tofauti na toleo la mwaka 2002 lililofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Amesema katika kutekeleza mradi huo Ofisi ya mwanasheria mkuu imeajiri mawakili wa serikali zaidi ya 50 na kuanzisha Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ambayo imekuwa kiini cha utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kitaifa.
Ameongeza kuwa urekebu wa sheria ni zoezi la kitaalamu linaloongozwa na misingi ya kisheria na lengo ni kuhakikisha sheria za nchi zinabaki kuwa hai, rafiki kwa mtumiaji na kuendana na wakati.
Kuhusu changamoto, Mh. Johari ametaja upungufu wa rasilimali watu na fedha, lakini amepongeza ushirikiano wa serikali uliowezesha mradi kukamilika kwa mafanikio.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Urekebu, Rais atatoa tamko rasmi la kutangaza tarehe ya kuanza kwa matumizi ya toleo hilo.
“Tumeishapendekeza Julai 1, 2025 kama tarehe rasmi ya kuanza kutumika ili kuruhusu usambazaji wake mapema,” alieleza.
Toleo hili jipya linatarajiwa kuwa chombo muhimu cha kusaidia maendeleo ya Taifa kwa kuweka msingi thabiti wa sheria unaoeleweka kwa wote.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini nakala 3 za Sheria za Tanzania zilizofanyiwa urekebu kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha Sheria ya urekebu wa sheria, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 23 Aprili, 2025.
Viongozi mbalimbali wakiwa katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel Maneno akishiriki katika hafla ya uzinduzi wa toleo hilo Ikulu Chamwino jinini Dodoma.