Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo Pichani) leo Aprili 25,2025 kuelekea uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania unaotarajia kufanyika Aprili 28,mwaka huu katika Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Na Alex Sona, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Benki ya Ushirika Tanzania(COOP Bank Tanzania) Aprili 28 mwaka huu jijini Dodoma.
Pia Rais Samia atatembelea makao makuu ya Benki hiyo na kukagua maonesho ya Ushirika yatakayofanyika kwenye viwanja vya ukumbi wa mikutano Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 25,2025 Jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi.Rosemary Senyamule,amesema kabla ya uzinduzi wa Benki, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa atazindua Kongamano la Kitaifa la wanaushirika Aprili 27 mwaka huu.
“Kongamano hilo litakuwa na mada kuu isemayo” Tafakuri na mijadala juu ya historia, changamoto na fursa za uwekezaji katika sekta ya Ushirika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuondoa umaskini,”amesema
Aidha amesema kuwa washiriki wa mkutano huo ni viongozi wa kitaifa,wadau wa ushirika kutoka ndani na nje ya nchi,Wafanyabiasha na wananchi wa kawaida.
Amesema kuwa Benki hiyo ni ya kipekee inayomilikiwa Kwa ubia na vyama vya ushirika,wanachama wao,vikundi vya kijamii na taasisi za ushirika kutoka Nchini.
“Benki hii yenye makao yake makuu hapa Dodoma imetupa heshima kwa jiji letu kama kitovu cha uongozi, utawala na Sera za kitaifa,Wananchi wa Dodoma wanayo nafasi ya kipekee kunufaika na fursa hii, “amesisitiza
Hata hivyo ametoa wito Kwa wananchi wote wa Dodoma na maeneo jirani kujitokeza Kwa wingi na uzalendo kushiriki katika tukio hilo la kihistoria.
“Huu ni mwanzo wa enzi Mpya ya kifedha Kwa wananchi wa kawaida kupitia benki wanayoimiliki wenyewe”.