Na Silivia Amandius – Kyerwa, Kagera
Katika muendelezo wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, wananchi wametakiwa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani imekuwa chanzo kikuu cha migogoro na uhalifu katika jamii.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kikukuru, April 24, mwaka huu Diwani wa kata hiyo, Mheshimiwa Yustus Tito Leopold, alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mikononi, hali inayochochea uhalifu kama mauaji na ukatili wa kijinsia.
“Kwa kweli katika kata yangu, matukio ya uhalifu yamekuwa ya mara kwa mara. Watu wanachomana moto, wanapigana, na hatimaye kujikuta wakifanya makosa ya jinai. Kupitia msaada huu wa kisheria, naamini matukio haya yatapungua kwa kuwa wananchi wanapata maarifa na uelewa wa kisheria,” alisema Diwani Yustus.
Aidha, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha kampeni hiyo inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu ya sheria na kufahamu wajibu wao wa kisheria na kikatiba.
Naye Afisa wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi, Bi. Getruda Mwiga, ambaye pia ni miongoni mwa watoa elimu ya kisheria katika kampeni hiyo, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa taratibu za kisheria, ikiwa ni pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahalifu baada ya kukamatwa.
“Wananchi wengi bado hawajui utaratibu wa mhalifu kukamatwa, kupelekwa wapi na kwa sababu gani. Elimu hii ni muhimu sana kwa jamii,” alisema Bi. Getruda.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuzingatia elimu waliyopatiwa na kuitumia kama nyenzo ya kupambana na vitendo vya kihalifu ambavyo vinakwamisha maendeleo ya jamii.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kikukuru, akiwemo Bw. Daniel Ruhinda, walitoa maoni yao wakisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa midahalo na mikutano ya aina hiyo ili kuendelea kutoa elimu kwa jamii. Pia walimshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji na vitongoji kwa kuwapatia elimu ya kisheria.