SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Idara inayohusu Sayansi na Teknolojia imetengeneza mwongozo wa matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika Taasisi zake za Elimu ya Juu ili iweze kuleta manufaa kwa watu wote.
Imesema hakuna namna ya kusema kuzuia, badala yake wanatengeneza utaratibu wa kuhakikisha inatumika vizuri.
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Prof. Peter Msofe amesema hayo leo Aprili 25, 2025 wakati akifunga maonesho ya wiki ya ubunifu ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam iliyokuwa na kauli mbiu “Kuelekea Mustakabali wa Ubunifu katika Afya.”
Prof. Msofe ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo ameipongeza MUHAS kwa kuongoza safari ya mageuzi. “Hili si tukio tu,” amesema, “ni harakati—harakati ya kuuweka ubunifu kuwa sehemu ya msingi ya maendeleo ya taifa letu, hasa katika sekta ya afya.”
Amesema bunifu mbali mbali zilizoonyeshwa na vijana chuoni hapo zimethibitisha kuwa wiki hiyo ya ubunifu ilikuwa si kwa ajili ya maadhimisho ya mawazo bunifu peke yake bali pia ni uthibitisho wa dhamira ya chuo hicho kuuweka ubunifu kama nguzo kuu ya shughuli zake.
Amesema afya ya mwanandamu ni jukumu la kila mtu lakini kuna mambo mengi sana yanatokea katika afya ambayo yanahitaji utatuzi mpya (new solution), hivyo kila mara kuna changamato ambazo zinatokea ambazo zinahitaji utatuzi
“Kuwepo na wiki ya ubunifu ni mojawapo ya kupata namna ya kushughulikia changamoto hizo na kupata majawabu mapya hivyo sisi kama Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na MUHAS kwa kutengeneza wiki ya kuwaleta wabunifu pamoja ili waje waonyeshe njia mbali mbali za kibunifu za kutatua changamoto zinazowakabili watanzania katika Afya.” Amesema Prof.Msofe.
Prof. Msofe amesisitiza kuwa mustakabali wa Tanzania uko mikononi mwa wabunifu wake—kuwapa nguvu, kushirikiana kwa dhati, na kuhakikisha maarifa yanatafsiriwa kwa vitendo.
Katika wiki hiyo pia bunifu tatu kutoka MUHAS zimetunukiwa Sh. milioni 20 kila moja kwa ajili ya kuendeleza mawazo yao hadi kufikia bidhaa inayoweza kuingia sokoni.
“Mafanikio haya si ya MUHAS pekee, bali ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja, mchanganyiko wa uongozi wa kiakademia, sera za serikali zenye maono, na msaada kutoka kwa wadau wa kimataifa wakiwemo washirika kutoka Sweden na Shirika la Maendeleo la Tanzania. Pia, wahitimu wa chuo hicho walionesha mshikamano wao kwa kuchangisha Sh milioni 10 kupitia mbio za hisani kwa ajili ya kuunga mkono kituo cha ubunifu.
Wiki ya Ubunifu ilijumuisha matukio mbalimbali yenye mvuto kama vile mashindano ya mawazo bunifu (ideathons), mashindano ya ubunifu wa kiteknolojia (hackathons), na ushindani wa uwasilishaji wa miradi (live pitch competitions), ambayo yalionyesha kiwango cha ubunifu na ari ya wanafunzi na jamii ya wasomi wa MUHAS. Pia, ilionyeshwa Kituo cha Kukuza Ubunifu cha kwanza kilichozinduliwa Oktoba 2023 katika Kampasi ya Mloganzila, ambacho bado kinawekwa vifaa lakini tayari kimetambuliwa kama alama ya matumaini kwa wabunifu chipukizi wa Kitanzania.
Wiki hii imehitimishwa kwa wito mzito kwa wabunifu na taasisi zote kuendelea kuvuka mipaka, kujenga ushirikiano mpya, na kukuza utamaduni wa ubunifu unaoweka ustawi wa jamii mbele.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema Chuo hicho kitahakikisha kinapeleka masuala ya bunifu katika maeneo mbali mbali ili kutatua changamato za wananchi na kuimarisha bunifu hizo.
Amesema mpaka sasa chuo kimeimarisha mifumo ya ubunifu, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Kitengo cha Ubunifu na Kituo cha Ukuaji wa Ubunifu (Innovation Hub) katika Kampasi ya Mloganzila.
Kituo hicho kimewezeshwa na wahitimu wa chuo waliotoa fedha zilizotumika kununua mashine ya kuchapisha kwa teknolojia ya 3D.
Aidha amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na serikali pamoja na wadau ili kuboresha miundombinu ya ubunifu, haki miliki, ushauri wa kibiashara, na ushirikiano wa kimataifa wa utafiti.
Amesema, Mradi unaotarajiwa kwa hamu ni hatua ya pili ya Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Moyo chenye teknolojia ya kisasa kama akili bandia (AI). Tukio hili limedhihirisha dhamira ya MUHAS katika kuendeleza ubunifu kwa ajili ya afya bora kwa jamii.
Tulikuwa na wiki ya bunifu hapa chuoni, tumeifanya kwa kuwafanyia vipimo wananchi vya magonjwa mbali mbali… wananchi kama 300 walijitokeza na pia tulialika taasisi mbali mbali na sekta binafsi za afya.
“Sisi kama Chuo Kikuu cha Afya tutahakikisha kwamba masuala ya bunifu yanaimarika… na kama mlivyoona kwenye mabanda mbali mbali bunifu ambazo mmeziona ni nyingi, vijana wamejikita kwenye kutafuta bunifu zenye kutatua na utambuzi wa magonjwa wanatafuta bunifu za kurahisisha uchunguzi wa magonjwa ambazo njia zake ama vifaa vyake viwe garama nafuu pia wanatengeneza bunifu kwenye upande wa dawa na jinsi hizi dawa zitakavyomfikia mwananchi na pia kuna bunifu kwenye vifaa tiba.
Amesema, serikali imewekeza sana kwenye hospitali zetu ukianzia hospitali za Wilaya, Mikoa na Taifa. Sasa ili vifaa tiba vifanye kazi vinahitaji kuendelea kuviimarisha na jinsi ya kuvitunza.
” Tutaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali tuna mradi mkubwa wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, mradi huu unajenga miundombinu ya chuo na kusomesha wataalamu ambao tunaamini watakuja kusaidia kwenye bunifu mbali mbali.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza katika hafla ya kufunga Wiki ya Ubunifu ya MUHAS iliyofanyika leo, Aprili 25 2025, katika Ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es Salaam.

Mfamasia John Method ambaye pia ni mbunifu akizungumza katika hafla ya kufunga wa Wiki ya Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyofanyika leo, Aprili 25, 2025, katika Ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es Salaam.