Na Mwandishi wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa watanzania wote kuuenzi muungano ili kudumisha amani, umoja na udugu waliotuachia waasisi wa taifa laTanzania; Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye huku akiwaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuimarisha usalama wa wananchi.
Wito huo ameutoa leo Aprili 26, 2025 katika maadhimisho ya sikukuu ya Muungano kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Sangambi wilayani Chunya mkoani Mbeya baada kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Mbeya yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 40 inayosimamiwa na TAMISEMI ambapo wananchi wamempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika miradi hiyo.
Miradi hiyo imejumuisha ujenzi wa Sokomatola kupitia mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya miji, ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya mkoa wa Mbeya, ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Lwanjilo kwa kutumia fedha za mradi wa SEQUIP, ujenzi wa Stendi ya Mabasi Chunya na ujenzi wa Kituo cha Afya kata ya Sangambi.
Waziri Mchengerwa ametoa wito kwamba kila mwaka mwezi wa Aprili ni vema kukawa na wiki maalum la muungano ambapo shule za msingi na sekondari kote nchini zifanye maonyesho ya sanaa, ngonjera, na mijadala kuhusu muungano ili kuendelea kuwapa uelewa zaidi wanafunzi ambao ni kizazi cha sasa kuhusu umuhimu wa muungano.
Pia Wasanii, Waandishi na Watayarishaji wa Filamu wahamasishwe kuandika simulizi za mapenzi, ujasiri na udugu kati ya vijana wa maeneo mbalimbali kama Unguja, Pemba, Dodoma na Kigoma kwa kutumia kiini cha Muungano.
Aidha, kila mwaka vijana kutoka pande zote mbili za muungano wakutane, wajadiliane, wajifunze, watoe maazimio yao kwa Serikali kuhusu namna bora ya kuulinda na kuuenzi Muungano huu.
Amesema ni muhimu kukumbuka kuwa, wakati dunia ikiliangalia Bara la Afrika likipitia misukosuko mikubwa ya kisiasa na kijamii kutokana na migogoro ya utaifa, mapinduzi ya mara kwa mara, hadi juhudi za mataifa mengi kujitenga na wenzao kwa misingi ya kikabila, kidini au kijiografia—Tanzania ilichagua na inaendelea kuchagua njia tofauti kabisa: njia ya amani, mshikamano na umoja.
Aidha, wakati mataifa mengine yakikumbwa na vurugu za ndani, vita vya wenyewe kwa wenyewe na harakati za kutengana ambazo zilisababisha na zinaendelea kusababisha maafa makubwa, Tanzania ilichukua hatua ya kishujaa ya kuungana, ambapo amesema muungano wetu haukuwa wa karatasi tu; haukuwa mkataba wa kisiasa usio na roho. Ulikuwa ni mapinduzi ya kiitikadi, kijamii na kimaadili. Uliwashinda wale waliotilia shaka uwezo wa watu kutoka tamaduni, dini, lugha na hata mazingira tofauti kuishi kwa pamoja kwa misingi ya kuheshimiana na kuthaminiana.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba kupitia Muungano huu, Tanzania imebarikiwa kuwa taifa la kwanza katika Afrika Mashariki na moja ya mataifa machache duniani lililovunja kuta za jinsia na kumpa mwanamke kiti cha juu kabisa cha uongozi wa nchi.
”Ndiyo! tumekuwa taifa la kwanza katika ukanda huu kumpata Rais mwanamke, Mama Samia Suluhu Hassan, kiongozi mashuhuri kutoka kisiwa ambacho wengine hawakutegemea kingezalisha rais wa kitaifa, tena wa jinsia ya kike!
Amesema kizazi cha sasa bado hakijatambua faida na umuhimu wa muungano huu hivyo wazazi wanajukumu la kuwaelimisha ili waweze kufahamu badala ya kuwalaumu.
Katika ziara hiyo Mhe. Mchengerwa aliambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera