KWA zaidi ya miongo mitatu, Tanzania imekuwa ikiimarisha mazingira yake ya biashara kupitia mageuzi ya kiuchumi na sera za kuvutia uwekezaji, ikiwa ni pamoja na uwekezaji wa ndani na wa kigeni. Hivi sasa, Tanzania ni kivutio kikubwa cha uwekezaji wa biashara za ubunifu, na huku macho ya Afrika nzima yakiwa kwenye uzinduzi wa Tanzania Impact Investment Forum 2025 (TIIF 2025), kongamano kubwa la kimataifa lililofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Kongamano hili la siku mbili, lililoandaliwa kwa mwaliko maalum na kuongozwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, limekusanya wawekezaji wa kimataifa, watunga sera, wajasiriamali, na watoa huduma wa maendeleo ya biashara. Likiwa chini ya kaulimbiu isemayo “Kuharakisha Ukuaji wa Biashara Kupitia Uwekezaji na Ubunifu,” kongamano hili limejidhihirisha kuwa ni jukwaa muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kufungua fursa za upatikanaji wa mitaji kwa biashara zenye malengo ya kijamii na kimazingira.
Afisa Mpango wa Kitaifa na Mchumi katika Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, Daniella Kwayu Raymond, amesema: “Tunajivunia kuweza kuandaa majukwaa kama haya. Kupitia warsha maalum, vyumba vya mikutano ya kidijitali (Deal Rooms), vipindi vya kutoa mawasilisho (Pitch Sessions), na maonesho, Kongamano hili limelenga kujenga mahusiano ya pamoja kati ya biashara bunifu na wawekezaji.”
Miongoni mwa vipengele muhimu vya kongamano hili ni Maonesho ya Ubunifu, yatakayonyesha miradi 15 bora ya wajasiriamali wa Kitanzania, ambapo wawekezaji watapata fursa ya kukutana ana kwa ana na waanzilishi wa biashara hizo. Pia, baadhi ya biashara changa zilizochaguliwa zitatoa mawasilisho ya moja kwa moja, yakionyesha mbinu zao za kukuza ujasiriamali nchini.
Kongamano hilo linajumuisha maeneo maalum ya kidijitali yanayoitwa Deal Rooms, ambapo wajasiriamali na wawekezaji hukutana kwa mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara. Daniella alisema, “Washiriki watapata mafunzo ya kipekee kuhusu mbinu bora za kuandaa mawasilisho ya kuvutia wawekezaji, kue]lewa taratibu za upatikanaji wa mitaji, na kukuza biashara zao kwa ufanisi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.”
Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuvutia wawekezaji tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mwaka 1997. Hii ilikuwa ni hatua muhimu katika kurahisisha taratibu za uwekezaji. Sekta mbalimbali kama kilimo, madini, utalii, nishati, na hivi karibuni teknolojia na biashara changa (startups) zimekuwa na mafanikio makubwa. Serikali ya Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuunda sera rafiki kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu, kuanzisha maeneo maalum ya kiuchumi (EPZs na SEZs), na kutoa motisha mbalimbali za kodi na kifedha.
Juhudi hizi zimeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi barani Afrika, na kupitia majukwaa kama TIIF 2025, inaonesha dhamira yake ya kuendeleza mwelekeo huu kwa kuunga mkono biashara bunifu na ujasiriamali wa vijana na wanawake.
TIIF 2025 ni sehemu ya Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Uswisi nchini Tanzania, unaolenga kuimarisha nafasi za kiuchumi kwa vijana na wanawake kwa kupitia taasisi imara, maendeleo ya sekta binafsi, na ushiriki jumuishi katika maendeleo ya taifa. Kongamano hili ni jukwaa la kimataifa lililobuniwa kukuza uwekezaji katika biashara changa bunifu nchini Tanzania, lengo lake likiwa ni kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi kupitia uvumbuzi na ujasiriamali.
Kwa zaidi ya miaka 40, Uswisi imekuwa mshirika thabiti wa maendeleo ya Tanzania, ikichangia ukuaji wa uchumi jumuishi, kuwezesha vijana, na kuimarisha mifumo ya utawala bora kwa maendeleo endelevu.
Baadhi ya wadau wa Uwekezaji wakiwa kwenye kongamano la TIIF, 2025.