Arusha- Tanzania
Mbunge wa Jimbo la Madaba na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Dkt. Joseph Kizito Mhagama, ameshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari yanayofanyika jijini Arusha wiki hii.
Akihutubia wadau mbalimbali wa sekta ya habari, Dkt. Mhagama ameelezea jitihada za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulinda na kukuza uhuru wa habari kupitia uundaji na maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.
Dkt. Mhagama alieleza kuwa Bunge limekuwa likichukua hatua kuhakikisha mazingira ya utendaji kazi wa waandishi wa habari yanazingatia weledi na maadili ya taaluma hiyo, amesisitiza kuwa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari yaliyofanyika mwaka 2023 yamekuwa hatua muhimu katika kuimarisha tasnia hiyo nchini.
“Marekebisho ya mwaka 2023 yamelenga kuhakikisha kila mwandishi wa habari nchini anakuwa na angalau kiwango cha elimu ya Stashahada (Diploma) katika fani ya uandishi wa habari, ndani ya kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa marekebisho hayo,” alisema Dkt. Mhagama.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa ukanjanja unaojitokeza katika tasnia ya habari na kuhakikisha kuwa habari zinazotolewa kwa umma zinazingatia uhalisia, weledi, na maadili ya taaluma, Vilevile, amewahimiza waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanazingatia matakwa ya kisheria ili kulinda heshima ya taaluma hiyo.
“Kwa kuimarisha taaluma, tunaimarisha tasnia. Tunalinda haki za waandishi lakini pia tunahakikisha jamii inapata habari sahihi, zenye ufanisi na zilizochunguzwa kwa kina,” aliongeza.
Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari mwaka huu yamewaleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wanaharakati, wanasheria, na wawakilishi wa serikali, huku mada kuu ikiwa ni kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya taifa.