Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akikagua mafunzo ya watendaji wa Uboreshaji ngazi ya Kata kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa leo Aprili 29,2025 ikiwa ni maandalizi kuelekea awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uwekaji wazi wa Daftari la awali la wapiga Kura. (Picha na INEC).
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba baada ya Mwenyekiti wa Tume kumtembelea ofisini kwake leo Aprili 29,2025. Jaji Mwambegele yupo mkoani Iringa kufuatilia utekelezaji wa awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari. (Picha na INEC).
…..
Na. Mwandishi wetu, Iringa
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili ya zoezi hilo litakalofanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura ambapo mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15 kuanzia mei mosi hadi saba mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Aprili 29,2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele wakati akizungumza na washiriki wa mafunzo ya siku moja ya watendaji hao ngazi ya Kata kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.
“Nawakumbusha tena kama nilivyowakumbusha katika zoezi lililopita, kwamba katika utekelezaji wa zoezi hili mzingatie sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, muwe wanyenyekevu kwa wateja mtakao kuwa mnawahudumia,”alisema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele amewaeleza watendaji hao kuwa wateja wengi watakaowahudumia ni wananchi wa kawaida hivyo hawana budi kuwahudumia vyema kwa lugha nzuri naikitokea kuna ulazima wa kuwarekebisha pale wanapokosea basi wafanye hivyo kwa staha.
“Zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kinachoipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa uchaguzi mkuu unaofuata,” alisema.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili utafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia tarehe 01 Mei, 2025 na kukamilika tarehe 04 Julai, 2025.
Uboreshaji wa Daftari unataraji kufanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza utajumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikao 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.
Mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ni pamoja na Iringa, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 1 hadi 7 mwaka huu.
Aidha, mzunguko wa pili utahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.
Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 04, 2025.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.
Katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.
Mambo mengine ni kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
Aidha, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa umma.
Lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa na litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza.
Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 na kukamilisha tarehe 25 Machi, 2025.